WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema msimamo wa Serikali wa kuzuia usafirishaji wa chakula kwenda nje ya nchi uko pale pale.
Pia amesema mahindi iliyokamatwa
mkoani Kilimanjaro yakisafirishwa kwenda nje ya nchi yataingizwa kwenye
Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) na magari yatabaki polisi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (
Alhamisi Juni 29, 2017) Bungeni mjini Dodoma wakati wa kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la
Mheshimiwa Ritha Kabati (Viti Maalumu) aliyetaka ufafanuzi kuhusu zuio
la kusafirisha mazao nje ya nchi kwa mikoa yenye chakula cha ziada.
“Tumedhibiti na kuzuia
usafirishaji wa chakula hasa mahindi kwenda nje ya nchi ili kuliepusha
Taifa kukumbwa na baa la njaa kutokana na baadhi ya mikoa kutopata
mavuno ya kutosha,”
“Kuna maeneo kama ya Sengerema na
Geita mahindi yamekauka, hivyo bado tuna upungu wa chakula. Na hata bei
ya chakula ipo juu, hatuna namna nyingine zaidi ya kudhibiti utokaji wa
chakula kwenda nje na nawasihi wananchi tushirikiane katika jambo hili,”
amesema.
Waziri Mkuu amesema kama
kunaulazima wa kusafirisha chakula kwenda nje ya nchi wahusika wakaombe
kibali katika Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi na kibali kiwe cha
kusafirisha unga na si mahindi.
Katika hatua nyingine Waziri Mkuu
amesema watumishi wote wa iliyokuwa Mamlaka ya Ustawishaji wa Makao Mkuu
Dodoma (CDA) waliokuwa wanaolalamikiwa na wananchi kutokana na utendaji
wao wataondolewa wakati wenzao wakihamishiwa Manispaa ya Dodoma.
Waziri Mkuu amesema kwa sasa
wanaendelea na ukaguzi na uhakiki wa kina kwenye masuala ya fedha na
utumishi ili waweze kujua CDA ilipovunjwa iliacha fedha kiasi gani na
shughuli zake zilifikia hatua gani ili ziendelezwe.
Amesema majukumu yote ya CDA
yatafanywa na Manispaa ya Dodoma na baada ya kukamilisha utaratibu huo
mpango kazi wote utaendelea kama ulivyopangwa.Kuhusu waliolipia viwanja
watakabidhiwa mara baada ya kukamisha utaratibu huo.
Waziri Mkuu alikuwa akijibu swali
la Mheshimiwa Matha Malata (Viti Maalumu) aliyetaka kupata tamko la
Serikali kuhusu wananchi ambao waliolipia viwanja CDA ambao bado
hawajakabidhiwa.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
ALHAMISI, JUNI 29, 2017.
Post a Comment