WANANCHI waliojichora
alama mbalimbali katika miili yao (Tatoo) wametakiwa kuchangia damu kama watu
wengine kwani hakuna uhusiano wa kisayansi kati Tatoo na uchangiaji damu.
Kauli hiyo imetolewa
leo Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya
Kikwete (JKCI), Prof. Mohamed Janabi baada ya kuzuka kwa upotoshaji juu ya watu
waliojichora Tatoo kuwa hawaruhusiwi kuchangia damu.
Profesa Janabi amesema
kuwa damu inapochukuliwa kwa mwananchi lazima ichunguzwe ili kuonekana kama iko
sawa kwa ajili ya kutumia kwa wagonjwa wenye upungufu wa damu hivyo zoezi hilo
halijalishi mwananchi ana Tatoo au hana.
“Wananchi wanatakiwa
waelewe kuwa kinachoambukiza magonjwa sio Tatoo bali ni wale wadudu waliopo
katika damu hivyo tunawashauri wananchi wote waendelee kuchangia damu,”alisema
Profesa Janabi.
Alifafanua kuwa jumla
ya watoto takribani 150 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji wa magonjwa ya moyo
katika hospitali hiyo hivyo uchangiaji wa damu unahitajika ili kusaidia
utekelezaji wa suala hilo.
Kwa upande wake Mkuu
wa Wilaya ya Ilala, Sophia Mjema amesema
kuwa ni jambo la kushukuru kuona watu wanajitolea kwa hiari kutoa damu kwani
wamefanya jambo la maana katika kusaidia kuokoa maisha ya wengine.
“Suala la kuchangia
damu sio la mtu mmoja pia linatakiwa lifanyike kila siku kwa sababu hakuna mtu
anayejua lini ataumwa au kupungukiwa na damu mwilini hadi kupelekea ahitaji
damu kwahiyo yatupasa sisi wenyewe tuwe na uhiari wa kuchangia damu,alisema
Sophia.
Nae, Mkurugenzi wa
Huduma ya Tiba Shirikishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Praxeda Ogweyo
amesema kuwa kwa siku Hospitali hiyo inapokea jumla ya lita 50 mpaka 60 wakati
mahitaji ya hospitali yanayotakiwa ni lita 100 mpaka 120 kwa siku hivyo utoaji
damu bado ni changamoto kwa wananchi.
“Hospitali
inajitahidi kutoa elimu juu ya umuhimu wa kuchangia damu ambapo tumeunda timu kwa
ajili ya kuzunguka kwenye maeneo mbali mbali nchini ili kutoa elimu na
kuhamasisha wananchi kuchangia damu kwa manufaa ya maisha yetu sote,”alisema Praxeda.
Praxeda ametoa
rai kwa wananchi, wizara mbalimbali, mashirika, taasisi na shule kufika katika
kituo cha kutolea damu cha hospitalini hapo ili waweze kuchangia pia amewataka
watanzania kuamini kuwa damu inayotolewa na kitengo hicho ni salama kwa ajili
ya matumizi ya wagonjwa.
June,14 ya kila mwaka
ni Siku ya Uchangiaji Damu inayoadhimishwa Duniani kote, kwa Halmashauri ya
Ilala vituo vinavyotoa huduma ya uchangiaji wa damu ni Mnazi Mmoja, Hospitali
ya Taifa Muhimbili,Karume Mchikichini, Hospitali ya Amana pamoja na JKCI.
Post a Comment