Na Daudi Manongi,MAELEZO,DODOMA.
Serikali kupitia Wizara ya
Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo imesema kuwa inakamilisha mapitio ya
Sera ya Maendeleo ya Michezo ya mwaka 1995 ili kuhakikisha inaendana na
mahitaji ya sasa katika maendeleo ya michezo nchini.
Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri
wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia Wambura wakati
akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini Mhe.Cosato Chumi aliyetaka
kujua mipango ya Serikali katika kufufua mchezo wa Riadha Bungeni Mjini
Dodoma leo.
“Serikali kwa kushirikiana na
wadau inatekeleza programu mbalimbali za kuendeleza mchezo wa riadha
nchini ikiwemo Kilimanjaro Marathon,Bagamoyo Marathon,Heart Marathon na
Tulia Marathon ambayo hushirikisha wanariadha kutoka nje”,Aliongeza
Mhe.Wambura.
Aidha pamoja na hayo Mhe.Wambura
amesema kuwa Wizara yake kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu,Sayansi na
Teknolojia pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI imeendesha mashindano ya
UMISETA na UMITASHUMTA ambayo pamoja na mambo mengine yanalenga kuibua
na kuendeleza vipaji vya vijana wetu katika mchezo wa riadha.
Akizungumzia suala la miongozo ya
Kiserikali amesema kuwa Wizara yake inakamilisha taratibu za kuandaa
miongozo ya kiserikali ili kuwezesha wadau wote kuendesha shughuli zao
katika mazingira ya weledi na stadi bora za michezo.
Hata hivyo Naibu Waziri uyo
amesema kuwa nchi yetu imeanza kufanya vizuri katika mashindano ya
Riadha kama ilivyokuwa katika miaka ya nyuma kupitia kwa wanariadha wake
kama Francis Naal,Samson Ramadhani,Gidamis Shahanga,Juma
Ikangaa,Suleiman Nyambui na Filbert bayi na hivyo kuitangaza nchi yetu.
“Nchi yetu kwa sasa imeanza kupata
mafanikio katika riadha kupitia wanariadha wetu kama Alphonce Simbu
aliyeshinda medali ya dhahabu kwenye mashindano ya standard Chartered
Mumbai Marathon,Cecilia Ginoka Panga aliyeshinda Beijing International
Half Marathon na Giniki Gisamoda aliyeshinda Shanghai International Half
Marathon,wote hawa wanaitangaza nchi yetu vizuri na kuifanya ifahamike
na hivyo kuvutia watalii ”Alisisitiza Mhe.Wambura.
Post a Comment