Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Ghafla nimemkumbuka Manji


ABDUL MKEYENGE 

KILA pumzi wanayoipandisha na kuishusha watu wa Yanga wakati huu namkumbuka Yussuph Mahboub Manji. 

Ni Manji aliyewafanya watu hao wajihisi kuishi kwenye sayari yao bila isiyoguswa na kiumbe kingine. Manji aliyekuwa akibadili 'mchanga kuwa sukari' amejiweka kando. Amejiuzulu nafasi yake kama Mwenyekiti wa klabu. 

Hii si taarifa nzuri. Ni taarifa mbaya kuisikia ikipenya kwenye ngoma za masikio ya watu wa Yanga. Ni taarifa inayopaswa kuwekwa kando ili shuguli nyingine za klabu ziendelee. Muda huu ambao Simba na Mohamed Dewji 'MO' wanafanya kila waliwezalo sokoni kuimarisha kikosi, Yanga wamepoa kama maji mtoni.

Hii sio destruri yao. Mara zote dirisha la usajili linapofunguliwa wao ndiyo wanakuwa na jeuri ya kusajili kila staa wanayemtaka, wasiyemtaka ndiye anayeweza kusajiliwa na timu nyingine. Haya ndiyo yalikuwa maisha yao. Timu nyingi zililia na Yanga. Hata wapinzani wao Simba mara nyingi walilia. 

Lakini sasa wako kimya kana kwamba hawataki kusajili. Huu ni ukweli mchungu wasiotaka kuumeza kwenye vinywa vyao. Ukimya wao sokoni juzi ulimuibua kusikojulikana Katibu Mkuu, Charles Boniface aliyesema msimu huu wameamua kusajili kwa mtindo wa kimya kimya. Ni kweli Yanga ya kusajili kimya kimya?

Nafahamu kazi za watendaji wa kila taasisi ni kuilinda hadhi ya taasisi yake inayompa mkate wa kila siku, lakini hapa Mkwasa alihitaji kutokeza hadharani na kuzungumza ukweli wa mambo. 

Ukweli ambao ungemuweka huru. Ni kama wiki kadhaa zilizopita alivyotokeza na kuitisha michango kwa wanachama, mashabiki kuichangia klabu. Hiki ndiyo kipimo chake kukomaa kiungozi klabuni.

Kuna timu za kusajili kimya kimya na isionekane kama kuna doa. Lakini kwa hadhi ya Yanga tunayoijua tulizoea kuziona zile vurugu zao za kumdaka juu kwa juu mchezaji aliyekuwa anakuja kusaini Simba na kumficha kwenye hoteli moja ya kifahari, huku ikimnyemelea na mchezaji mwingine anayetaka kusajiliwa na Azam.

Lakini Mkwasa kutokeza na kusema wameamua kusajili katika hali ya ukimya, kuna kitu cha msingi anachowanyima kuwajulisha wenye Yanga yao ambao wakiambiwa zoezi la kuchangia usajili watachanga tu. Ile kauli mbiu ya Bishana mpaka kufa nyuma ya kadi yao ya Uanachama bado iko vifuani kwa Wanayanga. Wanakaa nayo, wanatembea nayo, wanalala na kuamka nayo. 

Kwa vyovyote vile watajichangisha tu kuinusuru klabu.
Mifumo yetu mibovu ya kuendeshea soka tuliyonayo nchini ndiyo inayofanya Manji aonekane kiumbe cha ajabu Yanga, Lakini Yanga inaweza kujiendesha bila kutegemea fedha ya yeyote yule kutoka mfukoni mwa mtu. Hata hao Simba wanaolitikisa soko la usajili kadri wanavyotaka hivi sasa ni kutokana na watu wawili wameamua timu isajili. 

Hali waliyonayo Yanga inawakera na hawajaizoea. Wanachokifanya ni kujikaza tu mbele yetu, lakini wakikutana wenyewe kwa wenyewe kwenye makundi yao ya Whatsaap huwa wanalikiri hili, lakini hawawezi kulikiri hili mbele yetu. Katika hali hii waliyonayo Yanga unaachaje kumkumbuka bwana mifedha Manji? 

Kama Yanga wakiweza kustahimili hili la usajili lipite bila Manji, wanaweza kuishi bila Manji. Lakini silioni hili likipita hivi hivi. 

Yanga wajivuni kama walivyo. Hakuna kitu kinachowakera kama kushuhudia Simba wakiuza kurasa za mbele za magazeti. Ukisoma magazeti unakutana na kichwa cha habari kisemacho"Simba yamalizana na Okwi, upande wa chini wa taarifa hiyo unaona taarifa inayosema Wazir Junior aota mbawa Jangwani" Unadhani wanapenda kusoma taarifa za namna hii? 

Wachezaji Pius Buswita, Wazir Junior, Salmin Hozza, Kenny Ally kwa pamoja waliotajwa kuingia rada za Yanga kwa ajili ya kusainiwa, lakini mpaka sasa hakuna hata mchezaji mmoja kati ya hao aliosaini Yanga. 

Mwanzo na mwisho wa usajili wa Wazir Junior uliishia kwenda makao makuu ya timu hiyo akiongozana na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji kaka yangu Salum Mkemi akaishia kupiga selfie na makombe, kesho yake Wazir Junior akaenda kusaini zake Azam. 

Inashangaza. Ina maana viongozi wa Yanga wamefikia hatua hii ya kuzunguka na wachezaji, kupiga nao selfie kisha waende kusaini timu nyingine kama Wazir? Kama Yanga inashindwa kumsainisha Wazir itamsainisha mchezaji gani mwingine?

Muda huu ambao Jonas Mkude, Abdi Banda na Ibrahim Ajib, wamemaliza mikataba yao Simba na bado hawajasaini mikataba mipya wakivutana na Simba, enzi za Manji nadhani wakati huu tungekuwa tunazungumza mengine.

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget