Kikosi cha wachezaji 22 wa timu
ya Tanzania ‘Taifa Stars’, kimesafiri na kufika salama nchini Afrika
Kusini kikitokea Dar es Salaam, Tanzania.
Timu hiyo iliyoondoka jana
Alhamisi Juni 22, 2017 kwenda Afrika Kusini kwa ndege ya Shirika la
Ndege la Rwanda, itakuwa huko kwa ajili ya michuano ya kuwania Kombe la
Castle Cosafa.
Taifa Stars inayodhaminiwa na Bia
ya Serengeti, itaanza kampeni za kucheza hatua ya Robo fainali kwa
kucheza na Malawi Jumapili, Juni 25, mwaka huu katika michuano hiyo
iliyoandaliwa na Baraza la Mpira wa Miguu la nchi za Kusini mwa Afrika
(Cosafa).
Tanzania si mwanachama wa Cosafa,
lakini imealikwa katika mashindano hayo na imepangwa kundi A na timu za
Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli,
Madagascar na Zimbabwe. Kinara wa kila kundi atakwenda moja kwa moja
hatua ya robo fainali.
Timu za Botswana, Zambia na
Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland tayari zimepangwa
hatua ya robo fainali hivyo zinasubiri vinara wawili kutoka makundi ya A
na B kuungana nazo kucheza robo fainali.
Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum
Shabani Mayanga, amesema kwamba anaichukulia michuano hiyo kwa umakini
na uzito mkubwa kwa wachezaji kuzidi kupata uzoefu wa mechi nyingi za
kimataifa kwa mwaka.
Kadhalika, kiufundi Mayanga
anachukulia michuano hiyo kama sehemu ya maandalizi makubwa ya mchezo
dhidi ya Rwanda wa kuwania kucheza nafasi ya kushiriki fainali za Kombe
la Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani – CHAN.
Mchezo huo wa kwanza utafanyika Julai 15, mwaka huu kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, jijini Mwanza.
Kikosi cha Taifa Stars kilichopo
Afrika Kusini kinaundwa na makipa Aishi Salum Manula (Azam FC), Benno
David Kakolanya (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar
FC).
Walinzi wa pembeni upande wa
kulia ni Shomari Salum Kapombe (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan
‘Kessy’ (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael
(Azam FC) na Hamim Abdulkarim (Toto Africans FC).
Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni
(Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Hassan Banda
(Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia
kuwa ni Himid Mao Mkami (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.
Kadhalika wako viungo wa
kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod
Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza
Ramadhani Kichuya (Simba SC).
Katika safu ya ushambuliaji wamo
Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid
Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na
Shabani Idd Chilunda (Azam FC).
Post a Comment