*Ataka TRA wafanye sensa ya majengo kwenye miji
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewataka maafisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato nchini (TRA) wakusanye
kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze kodi ya majengo wazee
wenye umri zaidi ya miaka 60.
“TRA ijipange kukusanya kodi
za majengo kuanzia Julai Mosi 2017. Katika kutekeleza jukumu
hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya majengo wazee wenye
umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama makazi yao,”
amesema.
Ametoa agizo hilo leo
(Alhamisi, Juni 22, 2017) wakati akizungumza na wananchi na viongozi wa
wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA, wilayani humo,
mkoani Geita.
Waziri Mkuu amewataka maafisa
hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya mjini na siyo vijijini
kwani kodi hiyo haiwahusu. “Msiende vijijini. Nyumba za nyasi au za
tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini. Piteni kwenye mitaa,
muainishe aina zote za nyumba zinazostahili kulipiwa kodi. Mkishafanya
sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha wananchi kulipia kodi hizo,”
amesema huku akishangiliwa.
Pia amewataka wananchi
wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe wanapewa risiti yenye
kiwango halisi walicholipia. “Ukipewa risiti uiangalie kama ina kiwango
halisi cha fedha uliyotoa. Kuna watu wachache wasio waaminifu wanaamua
kukupa risiti lakini imeandikwa bei ndogo kuliko ile uliyolipia, ukitoa
laki moja anakuparisiti ya sh 10,000.”
Mapema, akitoa taarifa ya
ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Charles
Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka jana na ulikamilika
Juni 12, mwaka huu.
“Ujenzi wa jengo hili
umegharimu sh. bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko kubwa la idadi ya
walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/2011 hadi kufikia watu
600 mwaka 2016/2017”, alisema.
Pia alisema wamejenga ofisi
hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa wilaya hiyo ambao
walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA ambako ni umbali wa
zaidi km.120.
Alisema hivi karibuni
watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara, Iringa, ikiwemo
kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi, Njombe na Manyara.
“Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa Kahama,” alisema.
Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya sh. trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, JUNI 22, 2017.
Post a Comment