Na Jonas Kamaleki- MAELEZO
Zaidi ya vijana 2340 wenye
umri wa miaka kati ya 16 na 37 wameamua kujiondoa kwenye mtandao wa
mazoezi ya kigaidi na kujisalimisha ili kuishi maisha ya amani na
maadili mema baada ya kukutana na ushauri wa Jopo laViongozi wa Kamati
ya kitaifa ya Maadili ,Amani na Haki za Binadamu kwa jamii ya dini
zote nchini.
Hayo yalisemwa leo na Mwenyekiti
wa Kamati ya kitaifa ya Maadili ,Amani na Haki za Binadamu kwa
jamii ya dini zote nchini, Askofu William Mwamalanga katika mahojiano
maalum na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Askofu Mwamalanga,
vijana hao kutoka vijiji mbalimbali vya vya huko Ikwiriri na Kibiti
wamesema walitumbukia kwenye uhalifu huo mwaka 2011 ambapo baadhi ya
viongozi wa dini moja kutoka jijini Dar e Salaam walipita kuhamasisha
vijana kujiunga nao na kuachana na DINI ya kiislamu na kujiunga na
mafundisho yanayotofautina na uislamu ya kuua viongozi wote na
wananchi ambao walikata kuliunga mkono.
Imeelezwa kuwa asili ya kundi
hilo ni mafundisho yanayopinga uislamu na limejikita kwenye wilaya za
Kinondoni, Temeke, Mbagala na Mikoa ya Tanga Kagera, Morogoro, Dodoma,
Lindi, Mtwara, Pemba, Tabora na Pwani. Kundi hilo limekuwa
likifundisha vijana kujiunga na ugaidi kwa muda mrefu katika maeneo ya
Songea, Tunduru, Ikwiriri, Kibiti, Dar es Salaam, Mwanza na Dodoma bila
hatua zozote za kuzuia, aliongeza Askofu Mwamalanga.
“Vijana hao wamekiri kuachana na
mtandao wa kundi hilo huku wakiwaomba viongozi wa dini ya kiislamu
nchini kukemea mafundisho ya kareti na ugadi kwenye baadhi ya misikiti”,
alisema Askofu Mwamalanga.
Aidha, Kiongozi huyo wa Dini
alisema kuwa kundi hilo lilikuwa linawahimiza wanafunzi wa shule za
msingi na sekondari wakiume na wasichana kuacha masomo na kuolewa
na wavulana kujiunga na kundi hilo na wengine kupelekwa nje ya nchi
kujiunga na shule za ugaidi hii ndiyo siri ya vijana wengi kwenye
mikoa hii kujiunga na mtandao huo na wengi kutoendelea na masomo.
Askofu Mwamalanga aliongeza kuwa
vijana hao wamempongeza Mkuu mpya wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon
Sirro kwa uthubutu wake na waledi wa wa kuifanya Rufiji na Ikwiriri kuwa
eneo la amani hii itasaidia hata wanafunzi kusoma kwa amani na hasa
wasichana wengi ambao wamepewa uja uzito na kutelekezwa na wengine
wapo jijini Dar es Salaam ambako wanaishi maisha duni kwa hofu ya
kuuliwa .
“Ninalaani vikali mafundisho
ya uhalifu kufundishwa kwenye nyumba za ibada na nawahimiza vijana hao
kuwa askari wa siri wa kufichua waharifu wote na kuwataka wale
waliojificha misituni kujisalimisha kama wenzao”,alisisitiza Askofu
Mwamalanga .
Aidha, Askofu huyo amewataka
watendaji wa Serikali ngazi ya Halmashauri wakiwemo wakuu wa wilaya
kuwapatia vijana ardhi na kuwakamata mara moja watu wanaoeneza elimu
ya chuki kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ni Twahuti jina linalomaanisha
kuwa Serikali hii siyo ya dola la kiislamu.
Kwa upande wao baadhi ya wazee
140 walioshiriki kwenye maombi na dua maalumu ya kuombea kukomesha
mauaji hayo wamekiri kuwa mauaji hayo hayana uhusiano wowote na dini
ya kiislamu wala siasa bali ni uharifu kama uharifu mwingine .
Hivi karibuni Serikali
imeimarisha ulinzi na usalama katika maeneo ya Ikwiriri na Rufiji pia
Kibiti ili kudhibiti mauaji yaliyokuwa yakijitokeza katika maeneo hayo.
Kwa sasa hali imetulia na amani inaanza kurejea.
Post a Comment