mwagala
Rais wa Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF), Jamal Malinzi amepokea kwa mshtuko na majonzi
makubwa taarifa ya kifo cha shabiki maarufu wa Young Africans, Ally
Mohammed anayefahamika zaidi kwa jina la Ally Yanga, kilichotokea jana
Jumanne Juni 20, 2017 kwa ajali ya gari iliyotokea mkoani Dodoma.
Katika salamu za rambirambi kwa
uongozi wa Young Africans, familia, ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu
Ally Yanga ambako Rais Malinzi amewaasa kuwa na moyo wa subira katika
kipindi hiki kigumu kwao na kwa huzuni amewafariji akisema: “Sisi sote
ni wa Mwenyezi Mungu, na kwake tutarejea.”
“Hakika nimeshtushwa na taarifa
za kifo cha Ally Yanga ambaye nimejulishwa kuwa kilitokea katika ajali
ya gari huko Dodoma. Kifo hiki kimefanya wanafamilia wa mpira wa miguu
kupoteza hazina ya hamasa popote pale uwanjani,” amesema Rais Malinzi.
“Binafsi nilimjua Ally Yanga
katika masuala ya mpira wa miguu hasa akishabikia Young Africans na timu
zote za taifa bila kujali kuwa ni Twiga Stars (Timu ya taifa ya
wanawake), Taifa Stars, Serengeti Boys au ile Ngorongoro Heroes,”
amesema Malinzi.
“Hivyo, nawatumia Young Africans
salamu zangu za rambirambi nikiwapa pole kwa kuondokewa na mmoja wa
mashabiki mwenye mvuto wa kipekee katika hamasa uwanjani, lakini pia
alikuwa akisapoti timu za taifa,” amesema Rais Malinzi.
Aidha, Malinzi amesema:
“Nawatumia pole wanachama wote wa Young Africans kwa kuondokewa na
Shabiki mahiri Ally Yanga. Nawapa pole pia familia, ndugu, jamaa na
marafiki ambao wamepoteza mhimili wao.
“Naungana nao katika msiba huu
ambao pia ni msiba wetu sote wanafamilia ya mpira wa miguu. Naungana nao
pia kumwomba Mwenyezi Mungu aiweke peponi roho ya Marehemu Ally Yanga.
Amina.”
Inna Lillah wa Innalillah Rajaun.
Post a Comment