Mgeni Rasmi Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akifuatilia jambo wakati wa
sherehe za 56 za kuwakubali na kuwasajiri, Mawakili wapya 248 mapema
hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya ndugu wa Mawakili wapya
wakisubiri zoezi la kuapishwa kwa ndugu zao mapema hii leo katika
viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Mawakili wapya wakisubiri zoezi la kuapishwa mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Mgeni Rasmi Kaimu Jaji Mkuu wa
Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma (wanne toka kushoto waliokaa) akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya Majaji na Mawakili wapya mara baada
ya kuwaapisha mapema hii leo katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar
es Salaam.
Picha na Eliphace Marwa -Maelezo
……………………
Na. Eliphace Marwa – Maelezo
29/06/2017
Kaimu Jaji Mkuu wa Tanzania Prof.
Ibrahim Hamis Juma amewataka Mawakili wapya kufanya kazi kwa kuzingatia
maadili ya taaluma ya uwakili na kutumia taaluma zao kwa kutoa msaada wa
kisheria kwa jamii.
Aliyasema hayo leo Jijini Dar es
Salaam wakati wa Sherehe za 56 ya kuwapokea na kuwaapisha Mawakili wapya
248 iliyofanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.
Aidha Kaimu Jaji Mkuu amewahimiza
Mawakili wapya kujiendeleza kitaaluma kwa sababu kuwa wakili sio mwisho
wa taaluma kwani wanahitajika kusoma sheria za nchi mbalimbali Duniani
ili kuweza kuingia mikataba ya kimataifa.
Alisema mawakili wapya wanatakiwa
washiriki katika kutoa haki, wawe waaminifu kwa mahakama na wateja kwani
wakienda kinyume haki itapotea.
“Mawakili wote wanatakiwa kuwa
waaminifu kwa wateja wanaowahudumia na kushirikiana na mahakama katika
kutoa haki na wasiwe mawakala wa rushwa bali wawe mawakala wa kutenda
haki,” alisema Kaimu Jaji Mkuu Prof. Ibrahim.
Aidha Kaimu Jaji Mkuu aliwataka
mawakili hao kufika maeneo ya nje ya mji ili wasaidie upatikanaji wa
haki kwani kumekuwa na changamoto kubwa ya mawakili katika maeneo ya nje
ya miji.
Naye Rais wa Chama cha Wanasheria
cha Tanganyika (TLS) Tundu Lissu amewataka Mawakili hao kutumia taaluma
hiyo katika kuisaidia jamii kujua haki zao na utawala wa sheria japo
kuna changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia ya sheria nchini.
“Napenda kuwatakia kila la kheri
mawakili hawa wapya ila niwaombe watumie taaluma hii kwa kuisaidia jamii
kujua haki zao pamoja na utawala wa sheria,” alisema Mh. Tundu Lissu.
Idadi ya mawakili walioapishwa leo imepelekea Tanzania kuwa na idadi ya zaidi ya mawakili 6300.
Post a Comment