SASA mashabiki wa Yanga wanaweza
kuanza kutuliza presha, baada ya straika wao, Donald Ngoma, kudai kuwa
kama mambo yakienda vizuri ataendelea kukitumikia kikosi chake hicho,
kilichomuibua kutoka FC Platinum ya nchini Zimbabwe.
Ngoma amemaliza mkataba wake na Yanga ambapo mpaka sasa hawajafikia makubaliano yoyote, lakini taarifa zinadai kuwa uongozi unafanya kila linalowezekana kuhakikisha wanambakisha mkali huyo wa mabao.
Licha ya kwamba Simba wanamvizia, lakini upo uwezekano mkubwa Yanga wakafanikisha mpango wake wa kumzuia asiende popote kama wakiweka mkwanja wa maana, kama mchezaji mwenyewe anavyotaka.
Rafiki wa karibu wa mchezaji huyo, alisema, straika huyo hajamalizana na timu yoyote mpaka sasa na kwamba kama Yanga wakiwahi njia itakuwa nyeupe kumbakisha.
“Ni kweli Simba wanamfukuzia sana huyu jamaa (Ngoma), lakini bado hakuna makubaliano yoyote ya mkataba, licha ya kwamba wenyewe wanataka kumsainisha miaka miwili, lakini pesa ndiyo inayoonekana kuwa kikwazo, lakini kama Yanga wakiwahi wanaweza kuharibu dili hilo.
“Unajua bado Ngoma anaipenda sana Yanga, lakini tatizo linaloonekana ni kama timu yake hiyo imeishiwa fedha, ndiyo maana mipango yao inakwama, nakwambia kama watafanya mazungumzo na yeye hata leo wanaweza kufikia makubaliano mazuri,” alisema.
Akizungumzia taarifa za mchezaji huyo kutimkia Afrika Kusini, rafiki huyo alikiri na kudai kuwa amekwenda kwa masuala yake binafsi, lakini pia anaendelea kufuatilia mipango yake ya kujiunga na Mamelod Sundowns.
“Mara kwa mara amekuwa akienda huko na hata kipindi kile alipokuwa majeruhi alikwenda, kuna masuala yake anayafuatilia na pia kama ile timu yake iliyokuwa ikimhitaji kipindi kile Mamelodi Sundowns, kama bado wanayo nia ya kumchukua atafanya hivyo, lakini nikuhakikishie Yanga wakikaza buti watambakisha,” alisema.
Ngoma ni moja ya wachezaji muhimu wa Yanga ambao mikataba yao imefikia tamati na anatajwa kutaka kuondoka, huku Simba pia wakihusishwa kuitaka saini yake na taarifa zinadai kuwa alishawahi kuzungumza na kigogo mmoja wa Wekundu hao wa Msimbazi, japo hawakufikia muafaka.
Post a Comment