MWAGALA
Afisa Afya Bw. Peter Alfred
(katikati) akikagua hati ya kusafiria ya Bw. Paluku Ngahngondi (kushoto)
Mkongo anayeishi Zambia, kabla ya kupanda ndege ya Fastjet kuja Jijini
Dar es Salaam. Kulia ni Afisa Afya Bi. Shukrani Nkonjeka akiwa kwenye
mashine maalum inayompima kila abiria anayepita mbele yake kwa kupiga
picha na kutoa mlio wa endapo anajoto kali la mwili.
Bi. Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya
akimpa maelezo kuhusiana na ugonjwa wa Ebola, mmoja wa wafanyakazi wa
Kiwanja cha ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), Bw. Fred Martin
(kushoto).
Bi Shukrani Nkonjeka, Afisa Afya
akiwapa maelezo yanayohusiana na ugonjwa hatari wa Ebola madereva wa
taxi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA).
Madereva wa taxi wa kiwanja cha
ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), wakipokea vipeperushi vyenye
maelezo mbalimbali yanayohusu ugonjwa hatari wa ebola kutoka kwa Afisa
Afya, Bi. Shukrani Nkonjeka
MAAFISA Afya toka kitengo cha
magonjwa ya dharura mkoa wa Songwe wameweka kambi kwenye kiwanja cha
ndege cha Kimataifa cha Songwe (SIA), ili kubaini abiria wenye dalili za
ugonjwa wa Ebola ulioibuka hivi karibuni kwenye nchi ya jirani ya
Jamhuri ya Demokrasia ya Kongo.
Kiwanja cha Kimataifa cha Songwe
kilichojengwa na Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) mwaka 2012
kinapokea abiria 500,000 kwa mwaka kutoka sehemu mbalimbali ndani na nje
ya nchi, ikiwemo nchi jirani za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. TAA
inahudumia viwanja 58 vilivyopo chini ya serikali.
Afisa Afya Bw. Peter Alfred
amesema wamefunga mashine maalum na ya kisasa kiwanjani hapo, ambayo
abiria akipita umbali wa mita tano hadi 10 inampiga picha na kuonesha
joto alilonalo mwilini, na endapo atakuwa na joto la nyuzijoto 37.5
mashine hiyo itatoa mlio wa kengele.
Bw. Alfred amesema abiria
atakayekuwa na joto hilo, atachukuliwa na kupelekwa eneo maalum
lililotengwa umbali wa mita 300 kutoka eneo la kiwanja cha ndege na
baadaye kupelekwa hospitali ya Rufaa ya Mbeya kwa ajili ya matibabu
zaidi.
Hata hivyo, amesema mbali na
kuangaliwa kwa abiria wenye joto kali la mwili, pia hukagua na kupata
maelezo binafsi kwa kujaza fomu maalum kwa abiria wote wanaopita kwenye
kiwanja hicho wakitokea kwenye nchi za Kongo, Guinea, Sierra Leone,
Mali, Nigeria, Liberia, Senegal, Marekani na Hispania kutokana na nchi
hizo ziliwahi kukumbwa na ugonjwa huo.
“Hadi sasa tangu zoezi hili
limeanza baada ya kupatikana kwa taarifa za ugonjwa kuwa hapo Kongo,
bado hatujapata mgonjwa mwenye dalili hizo na tunaendelea kuudhibiti
kwani hapa ni njia kuu kwa abiria wanaotoka Kongo ni wengi,” amesema Bw.
Alfred.
Bw. Alfred amesema ugonjwa wa
Ebola unasababishwa na virusi vya Ebola vinavyoingia mwilini mwa
binadamu na wanyama kupitia puani, masikioni na machoni, na huambukiza
kwa kugusa majimaji ya mwili toka kwa mtu aliyeambukiwa virusi hivyo,
yakiwemo matapishi, damu, jasho, mkojo, machozi, kamasi na mate.
Pia binadamu anaweza kupata
ugonjwa huu kwa kugusa au kuosha maiti ya aliyefariki kwa ugonjwa huu au
kugusa shuka, godoro, nguo na blanketi lililotumika na mgonjwa; pia
kuchomwa na sindano au vifaa visivyo safi na salama vilivyotumiwa na
mgonjwa wa ebola; au kula matunda yaliyoliwa nusu na wanyama na kugusa
mizoga au kula wanyama pori kama nyani, sokwe na popo.
Bw. Alfred amesema dalili za
ugonjwa huu zinaanza kujitokeza kati ya siku mbili hadi 21 baada ya
kupata maambukizi, ambapo mgonjwa hupata homa kali ya ghafla, maumivu ya
kichwa, maumivu ya mwili, misuli na viungo, vipele mwilini, kuvia damu
chini ya ngozi, kutokwa damu mdomoni, puani, masikioni, machoni,
kuharisha na kutapika kunakoweza kuambatana na damu.
Hata hivyo, Bw. Alfred amesema
ugonjwa huu hauna tiba maalum wala chanjo, lakini mgonjwa hupatiwa tiba
saidizi kulingana na dalili alizonazo kama vile kushusha homa na
maumivu, kuongezewa damu na maji mwilini na tiba lishe.
Bw. Alfred amesema wananchi
wanaweza kujikinga na ebola kwa kuepuka kusalimiana kwa kupeana mikono
au kukumbatiana, kuepuka kugusa majimaji yaliyotoka mwilini mwa mgonjwa
au kuosha maiti, kuacha kutumia godoro, shuka na nguo za mgonjwa na pia
wawahi haraka kituo cha kutolea huduma za afya endapo wataona dalili za
ugonjwa wa ebola.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA SHERIA NA MAHUSIANO, MAMLAKA YA VIWANJA VYA NDEGE TANZANIA.
Post a Comment