NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
CHAMA Cha Mapinduzi CCM
Zanzibar, kimeendelea kuweka wazi msimamo wake kuwa hakiwezi kukaa meza
moja na CUF kuzungumzia Uchaguzi wa mwaka 2015 na Serikali ya Umoja wa
kitaifa (SUK) bali kipo tayari kukaa na chama hicho kujadili changamoto
zinazowakabili wananchi.
Msimamo huo umetolewa na Naibu
Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dkt. Abdallah Juma Saadalla “Mabodi” katika
Mahojiano Maalum kuhusu masuala ya hali ya Kisiasa, Kiuchumi na Kijamii
nchini huko Afisini Kuu CCM Kisiwandui, Unguja.
Alisisitiza kwamba mjadala wa
mambo hayo, umefungwa toka Machi 20, mwaka 2015 katika Uchaguzi wa
marudio, hivyo kwa sasa CCM inasimamia serikali zake zitekeleze kwa
uhakika na haraka Ilani ya Uchaguzi wa mwaka 12015/2020, kwa wananchi
wote bila ubaguzi.
Dkt. Mabodi alisema kitendo cha
kuendelea kujadili Uchaguzi uliopita ambao mwanzo ulifutwa kisheria na
kurudiwa tena ni kudhalilisha Katiba ya nchi, jambo ambalo CCM haipo
tayari kwani Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dkt. Ali Mohamed Shein na Watendaji wake wameingia madarakani kwa
misingi ya Kidemokrasia Kanuni na sheria za nchi na Dunia yote inajua
hivyo.
Hoja hizo zimekuja baada ya siku
za hivi karibuni pindi ujumbe wa Ubalozi wa Marekani kufanya mazungumzo
na Chama hicho, na baadae baadhi ya Magazeti na Mitandao ya kijamii
kupotosha mazungumzo hayo kwa kudai kuwa upo uwezekano vya vyama hivyo
viwili kurudi katika meza ya mazungumzo kujadili Suala la Uchaguzi
uliopita na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).
Pia alisema Chama hicho kipo
tayari wakati wowote kuzungumza na Chama chochote cha kisiasa, na nchi
mbali mbali Duniani juu ya kujadiliana mikakati na mbinu endelevu ya
kutatua matatizo na kero za wananchi hasa wa baadhi ya Majimbo ya Pemba
yasiyokuwa na maendeleo licha ya kuwa na Wabunge wanaotoka CUF,
waliowasusia wapiga kura wao na mzigo wote kuwaachia Wawakilishi na
madiwani wa CCM pekee.
“ Naomba Wapinzani wetu waelewe
kwamba Zanzibar ina mihimili mitatu ya Dola ambayo ni
Serikali, Baraza la Wawakilishi na Mahkama, vyombo hivi vipo kisheria
vikiongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi
Dkt. Ali Mohamed Shein na Baraza lake la Mawaziri, sasa mnataka tujadili
nini tena.
Pia kwa lugha rahisi na
inayoeleweka zaidi ni kwamba Safu hiyo itaendelea kubaki madarakani
mpaka 2020, hakuna miujiza wala taifa lolote Duniani la kuingilia siasa
zetu za ndani”., alisema Dkt. Mabodi na kuwataka wanasiasa kuwa
wakweli na wenye utu na huruma za kupigania wapiga kura wao wawe na
maisha mazuri, na kuondokana na siasa za jino kwa jino, chuki na
migogoro.
Huduma za kijamii
Alisema serikali inayotokana na
CCM kupitia Dkt. Shein imeimarisha huduma za afya sambamba na kuongeza
vifaa tiba vya kisasa katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na Pemba
Hospitali ya Abdalla Mzee huku ikiboresha kitengo cha upasuaji wa
matatizo ya Uti wa Mgongo, Kichwa kikubwa, Mishipa ya fahamu na
saratani ya Ubongo matibabu hayo yote yanafanyika Zanzibar Mnazi Mmoja
bure.
Kwa upande wa sekta ya elimu
serikali imeimarisha ngazi za elimu ya Awali hadi Vyuo vikuu ambapo kwa
sasa inazalisha wataalamu wa fani mbali mbali hapa nchi huku wengine
wakipata mafunzo yao nje ya nchi.
Aidha kumeimarishwa Sekta za
Uvuvi, Ufugaji na kilimo cha kisasa ambapo wananchi wanapata huduma za
Pembe jeo na kwa gharama nafuu na bure kwa wakati mwingine , huku
wakilimiwa na Matrekta ya kisasa.
Kwa upande wa miundo mbinu ya
serikali imeongeza fursa za upatikanaji wa nishati ya umeme, ujenzi wa
viwanja vya ndege na bandari za kisasa na kuruhusu wawekezaji katika
usafiri wa baharini na makampuni ya ndege huku imejenga barabara za
kiwango cha lami Unguja na Pemba mjini na vijijini ili wananchi wapate
unafuu wa kutoa mazao yao mashambani hadi sokoni kwa urahisi.
“ Wabunge wote ndani ya Bunge la
jamhuri ya Tanzania wanapokea Mafao, sitahiki, mishahara na fedha za
majimbo sawa , lakini cha kusikitisha wenzetu wanaporudi majimboni
wanadai kuwa serikali ya CCM ndio yenye dhamana ya kutatua kero za
wananchi, sio kwamba tumechoka tunaendelea kufanya na tunafanya mpaka
katika makaazi yao.” Alisema Dkt. Mabodi na kuongeza kuwa wapinzani
wanakimbia majukumu yao kwa kutotekeleza yale waliyowaahidi wapiga kura
wao.
Hali ya Kisiasa Zanzibar.
Dkt. Mabodi alisema hali ya
kisiasa Zanzibar kwa ujumla ipo shwari licha ya kuwepo kwa changamoto
za baadhi ya wanasiasa kutokubali mambo mema yanayosimamiwa na CCM
katika utekelezaji wake.
Lakini alieleza kwamba Chama hicho
hakitochoka kuwaelimisha kwani baadhi yao tayari wameanza kuhama ndani
ya CUF na kujiunga na CCM, katika maeneo mbali mbali nchini na hivi
karibuni wamepokea wanachama Wapya zaidi ya 90 huko Jimbo la Makunduchi
waliovutiwa na Sera, na siasa za Chama Cha Mapinduzi, waliodai kuwa
wamechoshwa na sera za CUF zisizotekelezeka.
Alisema kwamba kila nchi duniani
ina mifumo yake ya kiutawala hivyo katika ulimwengu wa Kidemokrasia
lazima uwanja wa siasa uwe na faida na kasoro za hapo na pale kwani
sehemu yoyote yenye pande mbili zinazopingana kimisimamo lazima hayo
yatokee lakini ni mambo yanayozungumzika.
Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK)
Naibu Katibu Mkuu huyo, alisema
SUK iliwekwa na wananchi wa Visiwa vya Zanzibar na wakati ukifika
wakaamua wenyewe kuiondosha au ibaki na kueleza kuwa yeye sio mingoni
mwa fikra za wapinzani wanaoamini kuwa Utulivu na Amani
ya Zanzibar vipo kwa ajili ya mfumo huo bali anachokiamini ni
kwamba Wananchi wamekuwa waelewa zaidi na kupima katika uzani kuwa ni
siasa zipi wazifuate ndipo walipamua dhana hizo kwa kuzika siasa za
Chuki na Marumbano.
“ Kipindi tupo katika SUK Zanzibar
yalitokea matukio mengi ya kutisha Zanzibar ambayo kihistoria
hayakuwahi kutokea na huwa sipendi kuyakumbusha ila nitatoa mifano, kuwa
matukio hayo ni pamoja na kujitokeza vikundi vya Kihalifu kama Mbwa
Mwitu, viongozi wa dini kuuawa na kumwagiwa Tindi kali pamoja, kuchomwa
kwa Makanisa, kuchomwa kwa Matawi na Ofisi za CCM, uhalibifu wa
miundombinu na baadhi ya wananchi kuigomea serikali.” Alifafanua Dkt.
Mabodi na kuhoji kuwa vitendo hivyo wakati vinatokea Wenzetu tulikuwa
katika serikali Kitaifa SUK, hakuna hata kiongozi hata mmoja aliyekemea
wala kulaani uhalifu huo.
Siri ya CCM kuwa imara kwa miaka 4O.
Mwanasiasa huyo alisema kufanikiwa
kwa Chama hicho kunatokana na radhi za Wazee wa Chama hasa wale
walioasisi vyama vya ASP na TANU, ambao miongozo waliyoiacha mpaka sasa
bado inaimarishwa tena kwa mifumo ya kisasa.
Pia alisema kwamba sababu nyingine
ya kuaminika kwa chama hicho inatokana na muundo wake ambao
umejitawanya kuanzia ngazi za mashina ( Nyumba kumi) hadi Taifa zote
hizo zinakuwa na viongozi wanaochaguliwa Kidemokrasia hali ambayo ni
tofauti na vyama vingine vilivyojenga safu za uongozi kwa ngazi za juu
pekee.
Hali ya kiuchumi
Naibu huyo ambaye amewahi kufanya
kazi katika taasisi za kimataifa, alisema kwamba uchumi wa Zanzibar
unakuwa kwa kasi kutokana na usimamizi mzuri wa ukusanyaji wa mapato,
unaotokana na usimamizi mzuri wa sera za kiuchumi zinazoendana na
matakwa ya sasa ya kuelekea katika falsafa za Zanzibar yenye viwanda.
Aliwashauri wananchi kutumia
vizuri fursa na mazingira bora ya kimiundo mbinu yaliyowekwa na serikali
kwa kufanya kazi kwa bidii hasa zile za uzalishaji mali ili waweze
kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Aliwaomba Wananchi kuunga mkono
juhudi zinazofanywa na Marais wa pande zote mbili ambao ni Rais wa
Zanzibar , Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kasi zao nzuri za
kiutendaji juu ya maendeleo ya nchi.
Aidha alisema Zanzibar imepata
neema ya Uchimbaji na utafutaji wa rasilimali za Mafuta na gesi asilia
ambazo kwa sasa tayari zimeanza kwa nchi nzima, hivyo wananchi watoe
ushirikiano kwani fursa hiyo ni moja ya vitega uchumi muhimu vya
kitaifa, lakini wasisahau kujiimarisha katika sekta za Kilimo, Uvuvi na
Ufugaji.
Mgogoro unaoendelea ndani ya CUF kwa sasa
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema
hawezi kuzungumzia sana mgogoro huo kwani haubebi dhamira ya kutatua
kero za Wanzania, bali unaendelea kukuwa kutokana na baadhi ya viongozi
wa Chama hicho kugubikwa na uchu wa madaraka na Utawala huku wakisahau
kwamba fursa hizo zinatokana na majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.
Aidha alisema huu ndio wakati
mwafaka wa Watanzania kupima siasa za Vyama vya Upinzani na badala yake
wakafanya maamuzi sahihi ya kuviacha na kujiunga na CCM chama ambacho
kauli na vitendo vyake vinahimiza Amani, Mshikamano na Umoja sambamba na
kueneza sera za maendeleo kwa wananchi wote.
Post a Comment