WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amefanya ukaguzi wa miundombinu kwa ajili ya sherehe za miaka 53 ya
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kusema kuwa maandalizi yake yako
pazuri.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo
mchana (Jumatatu, Aprili 24, 2017) mara baada ya kupokea taarifa ya
maandalizi na kukagua Uwanja wa Jamhuri ambapo sherehe hizo zitafanyika
na uwanja wa Nyerere Square ambako zitafanyika burudani mbalimbali kama
sehemu ya maadhimisho hayo.
“Nilikuja kuangalia maandalizi ya
sherehe hizo yamefikia wapi, najua kutakuwa na maonyesho ya kijeshi
zikiwemo michezo na burudani kutoka Tanzania Bara za Visiwani,” alisema.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo
kuwakaribisha wakazi kutoka wilaya zote za mkoa wa Dodoma na mikoa ya
jirani wafike kwenye maonyesho hayo ambayo kwa mara ya kwanza katika
historia ya Tanzania yanafanyika mkoani humo.
“Tunatarajia wageni wengi kutoka
nje ya mkoa huu wakiwemo viongozi wastaafu wa kitaifa, waheshimiwa
mabalozi na wake wa waasisi wa Taifa hili, Mama Maria Nyerere na Mama
Fatma Karume. Pia tutawatambulisha rasmi ndugu zetu waliochanganya
udongo wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964,” alisema.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye
Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba sehemu
zilizobakia zitakamilika kabla ya kesho.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
- L. P. 980,
DODOMA.
JUMATATU, APRILI 24, 2017.
Post a Comment