Uongozi wa wilaya ya
Kibaha, mkoani Pwani ukisikiliza kero mbalimbali za migogoro ya ardhi
kutoka kwa wananchi huko makazi mapya, kitongoji cha Kimara, Msongola
Kibaha Vijijini.
Mzee Hendric Simba
,mkazi wa Ngeta akitoa kilio chake kutokana na mgogoro wa ardhi ambapo
ulisababisha uongozi wa wilaya ya Kibaha kwenda huko Makazi Mapya,
Msongola Kibaha Vijijini kusikiliza kero mbalimbali za migogoro ya
ardhi. (picha na Mwamvua Mwinyi)
………………
Na Mwamvua Mwinyi,Kibaha VijijiniSERIKALI ya wilaya ya Kibaha, imerejesha hekari 89 mikononi mwa serikali ya kitongoji cha Makazi Mapya Msongola ,kata ya Kawawa,Kibaha Vijijini kwa ajili ya huduma za kijamii ikiwemo kujenga shule, zahanati.
Ardhi hiyo imerejeshwa kwa wananchi baada ya kukaa kipindi kirefu pasipo kuendelezwa.
Aidha serikali hiyo imewataka wakazi wa makazi mapya Msongola kuacha kukumbatia ardhi kuanzia hekari moja hadi 50 -100 pasipo kuziendeleza .
Kwa mujibu wa taarifa kutoka serikali ya wilaya, ilisema hadi ifikapo June mosi mwaka huu, asiyeendeleza atapokonywa ardhi hiyo.
Nae afisa tarafa ya Kibaha Anatory Mhango akizungumza na wakazi wa kijiji cha Ngeta ,Kimara na makazi mapya,alikemea tabia ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuuza maeneo kinyume na taratibu kwa kujinufaisha wenyewe.
Afisa tarafa huyo, ambae alikuwa akikaimu nafasi ya katibu tawala wilaya ya Kibaha, alieleza, uongozi wa vijiji hivyo usioze ardhi ya vijiji kuanzia sasa.
Mhango alisema uuzaji huo holela unaofanywa na wenyeviti hao umekuwa ukisababisha migogoro baina ya mtu na mtu ama mtu na mwekezaji kutokana na kuuziwa eneo moja.
Alisema tabia hiyo imekuwa ikiwapa kero wananchi ambao wamekuwa wakiuziwa eneo moja wawili au kuuziwa mara mbili.
Katika hatua nyingine serikali ya wilaya hiyo, imekata mzizi wa fitina kwa kumaliza migogoro ya baadhi ya wakazi waliokuwa wakigombania ardhi,ikiwemo eneo la Hendric Simba.
Moja ya mgogoro uliokuwepo ni wa wakazi wanaoishi kijiji cha Ngeta ambao walikuwa wakililia warudishiwe ardhi yao ya asili iliyopo kitongoji cha Kimara , ilichukuliwa mwaka 1974 katika operesheni vijiji.
Wakazi hao wametakiwa kuridhika na ardhi waliomegewa eneo la kitongoji cha Kimara .
Hata hivyo wamerejeshewa eneo la makaburi yao ya asili ambapo watatakiwa wazungushie uzio ili lisiingiliane na maeneo waliyogawiwa watu wengine.
Awali mwenyekiti wa wakazi wa asili,Hendric Simba alisema wakati wa operesheni vijiji walihamishiwa katika kijiji cha Ngeta ambapo hawakuridhishwa kutokana na kupewa maeneo madogo yasiyolingana na waliyokuwa nayo awali.Mwenyekiti wa kitongoji cha Makazi Mapya,Omari Kipuga alisema kitongoji cha Kimara kimeanzishwa mwaka 2006 kutoka kitongoji cha Makazi Mapya ambacho kipo kihalali.
Alisema operesheni vijiji ilifanywa kisheria na wakazi hao walihamishwa na kupelekwa maeneo ya Ngeta,Dusinyara,kikongo na Mwanabwito.
Kipuga alibainisha, eneo la Makazi Mapya limezalisha kitongoji cha Kimara,kata ya Kawawa,limepimwa kisheria na maafisa wa halmashauri ya Kibaha lina hekta zaidi ya 2,000 na wakazi wanaoishi kisheria 1,500.
Post a Comment