Mkurugenzi Kinga na Elimu ya Afya
Zanzibar Dkt, Fadhil Mohd Abdalla akimkaribisha Naibu Waziri wa Afya
Harusi Said Suleiman kuzungumza na waandishi wa habari katika
maadhimisho ya siku ya Malaria Duniani katika ukumbi wa Wizara ya Afya
Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Bi.
Harusi Said Suleiman akizunguza na waandishi wa habari katika
maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano wa
Wizara ya Afya Mnazimmoja Mjini Zanzibar.
Mwandishi wa habari wa ITV/Radio
One Farouk Karim akiuliza swali katika maadhimisho hayo yaliyofanyika
kwa mkutano wa waandishi wa habari katika Wizara ya Afya Mnazimmoja.
Meneja Kitengo cha Kumaliza
Malaria Zanzibar Mwinyi Issa Khamis akijibu maswali ya waandishi wa
habari katika maadhimisho ya siku ya malaria yaliyoadhimishwa kwa
mkutano wa waandishi wa habari Wizara ya Afya Zanzibar
Picha na Makame Mshenga-Maelezo Zanzibar.
…………
Na Ramadhani Ali/Maelezo Zanzibar
Naibu Waziri wa Afya Harusi Said
Suleiman amesema pamoja na mafanikio makubwa katika kupambana na Malari
Zanzibar, bado shehia tano zinaendelea kutoa wagonjwa wa maradhi hayo
zaidi ya asilimia tano.
Akizungumza na waandishi wa habari
katika maadhimisho ya siku ya Malaria Dunia katika ukumibi wa mikutano
wa Wizara ya Afya Mnazimmoja, amezitaja shehia hizo kuwa ni Tumbatu
Jongowe, Miwani, Micheweni, Chukwani na Kiwengwa.
Hata hivyo amesema maambukizi ya
malaria katika maeneo hayo yanasababishwa na wasafiri wanaoingia na
kutoaka nje ya Zanzibar mara kwa mara ambapo mwaka jana asilimia 55 ya
wagonjwa waliogundulika walikuwa na tabia hiyo.
Amesema takwimu za Malaria
Zanzibar zinaonyesha mafanikio mazuri ambapo mtu mmoja kati ya watu mia
moja hupata ugonjwa huo katika jamii isipokuwa shehia hizo tano.
Naibu Waziri wa Afya amewataka
wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kujikinga na Malaria ikiwemo
kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kusafisha mazingira kwa lengo la
kuondosha mazalio ya mbu wanaoeneza maradhi hayo.
Ameongeza kuwa Serikali kwa upande
wake mwaka jana iligawa vyandarua 705,000 bila malipo na kufanya zoezi
la kupiga dawa nyumba za wananchi ya kukinga malaria bila ya kuangalia
vyeo vya wamiliki wa nyumba hizo licha ya kukabiliana na changamo nyingi
katika kazi hiyo.
Amesema baadhi ya wananchi
wamekuwa wakikataa kupigiwa dawa nyumba zao kwa madai kwamba zinawaletea
athari za afya jambo ambalo halina ukweli kwani dawa hiyo ni salama kwa
afya.
Amekubusha kuwa Sheria ya Afya ya
Jamii na Mazingira ya mwaka 2012 pamoja na mambo mengine inasisitiza juu
ya udhibiti wa mbu na mazingira hivyo wananchi watakaokataa kupigiwa
dawa sheria itawabana.
“Watu wanaokataa nyumba zao
kupigiwa dawa ya kukinga maluaria bila sababu za msingi zinazokubalika,
sheria hii itawabana na hatua muafaka zitachukuliwa dhidi yao, ”
alisisitiza Naibu Waziri.
Meneaja Kitengo cha kumaliza
malaria Mwinyi Khamis alisema Zanzibar imeweka mikakati ya kumaliza
kabisa malaria ifikapo mwaka 2023 hivyo juhudi za jamii na Wizara ya
Afya ni muhimu.
Amesema mwaka jana watu watano walibainika kufa kwa malaria Zanzibar wakiwemo watoto wawili wenye umri chini ya miaka mitano.
Mapema akizungumza katika mkutano
huo, Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Dkt. Fadhil Mohd amewashauri
wananchi wasikubali kula dawa ya malaraia bila kupimwa na kuthibitishwa
kuwa wanayo malaria.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasema Malaria bado ipo Zanzibar, chukua tahadhari.
Post a Comment