Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 30 Aprili 2017, amekutana
na kuzungumza na viongozi wa dini wa madhehebu mbalimbali na kuuagiza
viongozi wa mkoa wa Kilimanjaro kutatua kero zinazowakabili wananchi wa
mkoa huo.
Rais Magufuli ametoa agizo hilo
kufuatia malalamiko ya baadhi ya viongozi wa dini kueleza kero
zinazowakabili ikiwa ni pamoja na manyanyaso yanayofanyiwa na
wafanyakazi wa Wakala wa Maegesho ya magari mkoani humo.
Kufuatia malalamiko hayo, Rais
Magufuli amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
nchini TAKUKURU kuchunguza mkataba uliongiwa kati ya Manispaa ya Moshi
na Wakala wa Maegesho ya magari mkoni humo ili kujua uhalali wake kwani
kumekuwa na ubadhirifu mkubwa wa upotevu wa mapato yatokanayo na
makusanyo ya maegesho hayo.
” Uangalie ule mkataba wa
parking wa hapa Moshi,kama kuna ufisadi wowote peleka Mahakamani,lakini
haya ya administration kayaangalie wasinyanyase watu, huwezi hata
ukamuona sheikh unafunga gari lake,ukimuona Mchungaji na kola yake
unafunga tu ni ushetani,sasa saa nyingine wale vijana wanaofanya ile
kazi wanajisahau, hawaheshimu utu wa Watanzania” amesema Rais Magufuli.
Pia amemuagiza Mkurugenzi wa
Manisapaa ya Moshi kutoa kibali cha Ujenzi wa Kituo cha Uchunguzi wa
maradhi kilichoombwa na mwananchi mmoja mkoani humo ili aweze kuendelea
na ujenzi huo kutokana na kutopewa kibali hicho kwa muda mrefu.
Katika hatua nyingine, Rais
Magufuli amesema kutokana na Serikali kuzuia unywaji wa pombe aina ya
viroba idadi ya vifo katika mkoa wa Pwani imepungua kutoka 80 hadi 20 na
hata ajali za pikipiki maarufu Bodaboda nazo zimepungua nchini.
Aidha, Rais Magufuli ametaka
uongozi wa Wilaya ya Hai kufanya kazi bila kutishwa na madiwani ikiwa ni
pamoja na kubadili sheria ndogondogo wilayani humo ili kupunguza kero
za utitiri wa ushuru kwa wananchi.
Rais Magufuli ametoa maagizo
hayo wakati alipokutana na viongozi wa dini wa mkoa wa Kilimanjaro,
Vyama vya Siasa na watendaji wa Serikali mkoani humo na kula nao chakula
cha mchana kilichoandaliwa na mkoa wa Kilimanjaro.
Jaffar Haniu
Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU.
Moshi, Kilimanjaro.
30 Aprili, 2017.
Post a Comment