Na Husna Saidi-MAELEZO
Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu
Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kongamano la Kimataifa la
Jinsia na Usawa Katika Jamii lililoandaliwa na Chuo Kikuu Kishiriki cha
Elimu Dar es Salaam (DUCE) Aprili 27 mpaka 28 mwaka huu chuoni hapo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es
Salaam na Afisa Habari, Elimu na Mawasiliano wa Chuo hicho Lila Mandu
alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu lengo la kongamano
hilo.
Mandu alisema lengo kuu la
kongamano hilo ni kuchunguza kwa kina masuala mbalimbali ya kijinsia
pamoja na kubaini mbinu bora za kuondoa ukosefu wa usawa wa jinsia
katika muktadha wa Taasisi za Elimu ya Juu.
“Tutatathmini sababu na changamoto
zinazosababisha ukosefu wa usawa wa kijinsia katika Taasisi za Elimu ya
Juu kwa kutumia mifano mizuri kutoka Taasisi zingine ambazo
zinajitahidi kuhamasisha usawa na haki za wanawake na wanaume pia,”
alisema Mandu.
Aliendelea kwa kusema kuwa
kongamano hilo litabainisha fursa za kimkakati katika kuwahusisha wadau
wa masuala ya jinsia katika kuhamasisha usawa na haki za watu wote
ambapo litakuwa na washiriki 140.
Aliwataja washiriki hao kuwa ni
wasomi kutoka DUCE, Taasisi na vyuo mbalimbali ndani na nje ya nchi,
wanafunzi wa shahada za uzamili na uzamivu katika masuala ya jinsia,
wawakilishi wa mashirika ya haki za binadamu, watunga sera pamoja na
wasomi wanaotambulika Kimataifa katika masuala ya jinsia.
Kwa upande wake, Mratibu Kitengo
cha Jinsia DUCE Fatma Hamad alisema licha ya maovu wanayotendewa
wanawake kuendelea kujitokeza hapa nchini, kongamano hilo litasaidia
kutoa elimu ya jinsia na usawa ili kusaidia Serikali na wananchi kwa
ujumla kuondokana na hadha hiyo.
Chuo cha DUCE pamoja na waandaaji
wa kongamano hilo wamealika wadau mbalimbali wa masuala ya jinsia,
wasomi, waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla kushiriki katika
kongamano hilo.
Post a Comment