Kamati za maji za visima kumi vya
maji katika manispaa ya Singida zimekuwa sababu ya miradi hiyo
iliyokamilika kwa asilimia miamoja kutofanya kazi na kuwanufausha
wananchi huku ikiwa imegharimu fedha nyingi za serikali na wahisani hasa
benki ya dunia.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi mwishoni mwa wiki hii mara baada ya
kukagua miradi hiyo na kujiridhisha kuwa miradi hiyo imekamilika licha
ya kutofanya kazi.
Dkt. Nchimbi amesema sababu kubwa
ya kutofanya kazi miradi hiyo ni udhaifu wa kamati za maji na wanasiasa
katika maeneo ya miradi kutojali shida ya wananchi ya kukosa maji na
hivyo kuitelekeza miradi hiyo badala ya kuisimamia.
Amesema lengo la miradi hiyo ni
wananchi wapate maji safi na salama kwa umbali usiozidi kilometa nne
kama ilivyoagizwa na serikali.
“Katika ukaguzi wangu nimebaini
mifumo katika miradi hii ya maji ipo vizuri sana. Baadhi inaendeshwa kwa
umeme na mingine kwa mafuta ya dizel. Makubaliano yalikuwa baada ya
kukamilika miradi hii iendeshwe na kamati za maji kwa asilimia mia
moja”, amesema.
Dkt. Nchimbi amesema wajibu wa
kamati hizo ni pamoja na kukusanya fedha zinazotokana na kuuza maji kwa
wateja pamoja na matengenezo ya miundombinu ya visima hivyo ili miradi
hiyo iwe endelevu.
“Fedha zinazopatikana ndizo
zitakazoendesha mradi husika ikiwemo kugharamia matengenezo ya mashine,
pampu, miundombinu, kununulia dizel, umeme na kumlipa mhudumu wa mradi.
Makubaliano ni miradi ikikamilika inabaki mikononi mwa wananchi kupitia
kamati zao za maji. Serikali na wafadhili hawatahusika tena”,
amesisitiza Dkt. Nchimbi.
Dkt. Nchimbi amesema serikali na
benki ya dunia imegharamia fedha nyingi kwenye miradi hiyo hivyo haiwezi
kuendelea kuona miradi inabaki kuwa mapambo badala ya kuwaondolea
wananchi kero ya maji.
“Naagiza wananchi wajipange upya
chini ya kamati zao wachague jumuiya za watumiaji maji. Kwenye jumuiya
hizo za maji wanaweza kuwepo pia wale waliokuwa kwenye kamati za awali
za maji. Jumuiya hizi ziwajibike kikamilifu zihakikishe zinapata fedha
kutokana na mauzo ya maji ili waendeleze miradi hiyo kwa ufanisi”,
amesema Dkt. Nchimbi.
Akiijengea nguvu hoja yake hiyo
amesema kuanzia mei mwaka huu anataka kuona kila wananchi wa manispaa
ya Singida,anapata maji safi na salama kwa umbali mfupi.
“Rasilimali maji ni msingi kwa
maisha ya viumbe hai wakiwemo binadamu. Maji yakiwepo tena kwa umbali
mfupi mambo yote yatakwenda vizuri. Maji yanasaidia kuweka mazingira
safi na afya za wananchi zinaboreka. Maji yana mchango mkubwa kwa jamii
inayoelekea kwenye Tanzania ya viwanda”, amesema.
Wakati huo huo, Mkuu huyo wa Mkoa
amesema kuwa wanatarajia baadhi ya miradi na hasa ile ya umeme
kuibinafisha kwenye mamlaka ya maji safi na maji taka (SUWASA) kwa ajili
ya kuiendesha. Mingi itaendelea kumilikiwa na wananchi wenyewe.
Awali mhandisi wa maji manispaa
ya Singida Max Hassan Kaaya amesema wanaendelea kuelimisha jamii kuwa
miradi hiyo ya maji ni mali yao hivyo jukumu la kuiendesha ni lao. Pia
wanapaswa kuilinda na kuitunza vizuri.
Naye mkazi wa kijiji cha Mtamaa
Hongoa Bunka amesema elimu zaidi itolewe ili kubadilisha fikiri potofu
ya baadhi ya wananchi kuwa jukumu la kuendesha miradi ya maji ni la
serikali. Wabadilike na kutambua kuwa ni mali yao na wao ndio
watakaoiendesha.
Post a Comment