Na Husna Saidi na Nuru Juma- MAELEZO
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imekusanya Trilioni 10.87 mpaka kufikia Machi mwaka huu kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Hayo yamesemwa na Kamishna Mkuu
wa Mamlaka hiyo Charles Edward Kichere wakati wa mahojiano na
mtangazaji wa TBC1 Rashid Salum katika kipindi cha Tunatekeleza
kinachorushwa kila siku za Jumatatu saa moja kamili jioni na Alhamisi
saa tatu na nusu usiku.
Kichere alisema, mwaka huu wa
fedha 2016/2017 TRA inatakiwa kukusanya Trilioni 15.105 na hadi kufikia
Machi mwaka huu TRA imefanikiwa kukusanya Shilingi Trilioni 10.87.
Aliendelea kwa kusema kuwa mpaka
kufikia Juni mwaka huu TRA itahakikisha inatimiza lengo la kukusanya
Shilingi Trilioni 15.105 ili kusaidia Serikali kuleta maendeleo kwa
wananchi wake.
Alisema kuwa TRA ina waajiriwa
wapya ambao wamepewa mafuzo ya miezi sita katika chuo cha kodi juu ya
mifumo mbalimbali ya ukusanyaji kodi ambao waliajiriwa moja kwa moja na
mamlaka hiyo kwaajili ya kutekeleza majukumu ya ukusanyaji kodi ndani
ya nchi.
“Tunatumia mfumo wa Tehama
kukusanya kodi na mifumo mingine mbalimbasli kama vile Tigo Pesa ,
Airtel Money na MPesa ili kurahisishia watu kulipa kodi wakiwa nyumbani
na kuepuka usumbufu,” alisema Kichere.
Kichere aliongeza kuwa kwa mwaka
huu wa fedha mapato yameongezeka mpaka kufikia asilimia 9.9 hadi 10
licha ya kuwa kuna baadhi ya maeneo hawakuweza kukusanya.
Aidha Kichere alisema Mamlaka kwa
sasa imejipanga kuwa na mahusiano mazuri na wafanyabiashara ili
kuhakikisha wafanyabiashara wanalipa kodi stahiki na kwa mujibu wa
sheria bila kutumia nguvu au uonevu wowote.
Hata hivyo mamlaka hiyo imekuwa
ikitoa elimu kwa walipa kodi kwa kupitia vyombo mbalimbali vya habari,
kutoa semina kwa watumishi wa umma , kuandaa makongamano ambayo yanatoa
elimu, kupitia mitandao ya kijamii na ziara mbalimbali ambazo wamekuwa
wakizifanya ili kuhakikisha wafanyabiashara wanapata elimu pamoja na
kujua wajibu wao katika kulipa kodi ili kuleat maendeleo nchini.
Post a Comment