Na Lydia Churi- Mahakama
Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2019/2020) pamoja
na Mradi wa Maboresho ya huduma za Mahakama, imepania kuhakikisha kuwa
kesi zote za zamani pamoja na zile zinazosajiliwa zinamalizika ili
wananchi waweze kuwa na kujenga imani zaidi na chombo hicho muhimu cha
utoaji wa haki nchini. Katika kulitekeleza hili, ipo mikakati iliyowekwa
na Mahakama kwa ujumla na ile inayowekwa na kila Kanda ya Mahakama Kuu
nchini.
Mikakati ya Mahakama ni pamoja
na Majaji na Mahakimu kupangiwa idadi ya kesi watakazotakiwa
kuzisikiliza na kuzimaliza katika kipindi cha mwaka mmoja. Kila Jaji
amepangiwa kumaliza kesi 220 kwa mwaka na kila hakimu anatakiwa
kusikiliza kesi 250 kwa mwaka. Mkakati mwingine wa jumla ni kiwango cha
muda kilichopangwa kwa kesi kukaa Mahakamani, mathalani, Mahakama ya
Tanzania imepanga kuwa kesi zote zilizosajiliwa Mahakama Kuu zisikae
Mahakama kwa muda unaozidi miaka miwili wakati katika Mahakama za Hakimu
Mkazi pamoja na zile za wilaya imeamuliwa kesi isizidi miezi 12
Mahakamani. Kesi katika Mahakama za Mwanzo inatakiwa kumalizika katika
kipindi cha miezi sita.
Aidha, Mahakama imeanzisha
utaratibu wa kufanya vikao na wadau wake ili kujadili namna ya kumaliza
kesi kwa wakati kama moja ya mikakati yake ya kuhakikisha kesi zote za
zamani zinamalizika Mahakama na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa
wakati ili kutimiza wajibu wake wa kikatiba wa kuwapatia wananchi wa
Tanzania Haki sawa na kwa wakati.
Pamoja na kuwepo kwa mikakati
ya Mahakama ya kumaliza kesi zilizoko Mahakamani, Mahakama Kuu kanda ya
Tanga nayo imejiwekea mikakati yake ili kuhakikisha inaenda sambamba na
kasi ya Mhimili huo ya kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati
kwa kumaliza kesi zao kwa wakati.
Akizungumzia suala la
kumalizika kwa kesi kwa wakati, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu kanda ya
Tanga Mheshimiwa Imani Abood alisema kanda yake imepanga kuwanunulia
Mahakimu wake wote (68) kompyuta Mpakato (Laptops) zitakazowasaidia
katika kurahisisha kazi zao na kuondosha mashauri kwa wakati katika
Mahakama mbambali za mkoa wa Tanga. Alisema lengo ni kuhakikisha
Mlundikano wa kesi zilizopo Mahakamani unaisha na pia kesi zinazosajiliwa zinamalizika kwa wakati.
Jaji Mfawidhi alifafanua kuwa
kompyuta hizo zitawasaidia waheshimiwa Mahakimu katika kuandika hukumu
ili wananchi waweze kupati haki kwa wakati. Aliongeza kuwa hivi sasa
Mahakimu wa mahakama za Mwanzo huandika hukumu kwa kalamu na baadaye
hukumu hizo hupelekwa kwenye mahakama za wilaya ambapo kuna umeme kwa
ajili ya kuchapwa na baadaye hurudishwa kwenye kwenye Mahakama za
Mwanzo.
Alisema pia kanda yake
inakabiliwa na uhaba wa watumishi hasa Makatibu Muhtasi pamoja na
vitendea kazi jambo ambalo limekuwa likichelewesha utolewaji wa hukumu
pamoja na upatikanaji wa nakala za hukumu kwa wakati. Aliongeza kuwa kwa
Mahakimu kupatiwa kompyuta hizo kutarahisisha upatikanaji wa haki.
Pamoja na kuwapatia Mahakimu
Kompyuta, Jaji Abood alisema Mahakama Kuu Kanda ya Tanga inao mpango wa
kuhakikisha inazipatia umeme baadhi ya Mahakama za Mwanzo kupitia Mradi
wa Umeme vijijini (REA) ili kurahisisha upatikanaji wa nakala za hukumu
kwa wakati. Na hivi sasa tayari Mahakama za Mwanzo tano zimeshapatiwa
umeme.
Jaji Abood aliitaja mipango
mingine iliyowekwa na Kanda yake katika kuitekeleza nguzo ya pili ya
Mpango Mkakati wa Miaka Mitano wa Mahakama ya Tanzania ya kuwapatia
wananchi haki kwa wakati kuwa ni kuwapeleka Mahakimu wenye kesi chache
kwenye Mahakama zenye kesi nyingi na upungufu wa Mahakimu ili
kuhakikisha mashauri yote ya muda mrefu yanaondoshwa na yaliyofunguliwa
yanamalizika kwa wakati.
Aliitaja mikakati mingine
waliyojiwekea ili kuondosha mlundikano wa kesi Mahakamani kuwa ni pamoja
na Majaji na Mahakimu kugawana idadi sawa ya Mashauri yaliyopo
Mahakamani, kutenga vipindi maalum vya kumaliza kesi zote, Mahakimu
wenyewe kufanya kazi ya kuchapa hukumu ili kesi zimalizike kwa wakatina
kufanya vikao na wadau ili kuweka mikakati ya kumaliza kesi kwa wakati.
Kuhusu utekelezaji wa Mpango
Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania kwenye kanda ya Tanga,
Jaji Mfawidhi alisema kuwa utekelezaji wa Mpango huo unaendelea vizuri
baada ya kuwa wamejiwekea mikakati ya utekelezaji. Alisema hivi sasa
kuna mageuzi makubwa kwenye Mahakama za
Mwanzo hasa zile zenye umeme.
Nakala za hukumu zinapatikana kwa wakati (ndani ya siku 21) na, mienendo
ya kesi ndani ya siku 90 ikiwa ni pamoja na kesi kumalizika kwa
wakati.
Kuhusu maendeleo ya Mradi wa kupambana na Rushwa ndani ya Mahakama (STACA), Jaji Mfawidhi anasema Mradi huu wa Mahakama ya Tanzania umeleta mageuzi makubwa ndani ya Mahakama hasa Kanda ya Tanga kupitia vifaa vilivyosambazwa (pikipiki, baiskelimabango na simu). |
Alisema kuwa suala la mapambano
dhidi ya Rushwa ndani ya Mahakama linatiliwa mkazo na Mahakama Kuu kanda
ya Tanga. Watumishi wa kanda hii wamekuwa wakikumbushwa mara kwa mara
juu ya kufuata maadili katika kazi zao na kuepukana na vitendo vya
rushwa. Alisema kufuatia mabango yaliyosambazwa na Mahakama katika
Mahakama za Mwanzo zote, Mahakama za wilaya, mahakama ya |Mkoa, mahakama
kuu, ofisi za halmashauri na ofisi za wakuu wa wilaya, jamii imeanza
kubadilika kimtazamo kuhusu Mahakama akisema hivi sasa malalamiko
yamepungua kwa kiasi kikubwa katika kanda yake.
Taarifa ya malalamiko ya mwezi
Februari 2017 inaonyesha kulikuwa na malalamiko 3 tu kwa kanda nzima
ikilinganishwa na malalamiko 11 yaliyokuwepo kipindi cha mwezi Januari,
2017 na malalamiko 15 katika kipindi cha mwezi Septemba, 2016.Kusambazwa
kwa vifaa kama vile Pikipiki na Baiskeli kumesaidia Mahakamu kuweza
kutembelea Mahakama za Mwanzo zenye idadi kubwa ya kesi na kuzimaliza
hivyo kusaidia kumaliza mlundikano wa kesi.
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji
wa Mahakama Kuu kanda ya Tanga, Afisa Utumishi wa Kanda hiyo, Farid
Mnyamike alisema hivi sasa wanaendelea na ujenzi wa Mahakama ya Mwanzo
ya Magoma iliyoko Korogwe pamoja na ukarabati wa jengo la Mahakama ya
Mwanzo ya Old Korogwe. Alisema kazi hiyo inafanywa na mkandarasi, SUMA
JKT ambaye kwa sasa amefikia zaidi ya asilimia 70 ili kukamilisha kazi
hiyo. Mkandarasi alikabidhiwa kazi hiyo Februari 2, 2017 na anatarajiwa
kukamilisha kazi hiyo ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu
alipokabidhiwa. Aidha, Mradi wa Ukarabati wa majengo ya Mahakama Kuu
tayari umekamilika na majengo yalishakabidhiwa kwa Mahakama ya Tanzania.
Mahakama kuu kanda ya Tanga pamoja
na kanda nyingine zinakabiliwa na tatizo kubwa la kuwa na miundombinu
mibovu hasa kwa upande wa majengo ya Mahakama nyingi za Mwanzo. Mahakama
Kuu kanda ya Tanga inayo majengo 68 ya Mahakama ambapo Mahakama 30
ndizo zinazofanya kazi wakati 12 ni zile zinazotembelwa na Mahakama 26
hazifanyi kazi kabisa.
Katika kutatua tatizo la ukosefu
na uchakavu wa majengo ya Mahakama nchini, Mahakama ya Tanzania
inatarajia kukamilisha miradi ya ukarabati na ujenzi wa majengo 70 ya
Mahakama katika kipindi cha miaka miwili ili kusogeza karibu huduma ya
utoaji haki kwa wananchi. Majengo tisa ya Mahakama kuu yanatarajiwa
kujengwa na kukamilika katika mikoa tisa ndani ya kipindi cha miaka
miwili.
Akizungumza wakati wa
Maadhimisho ya siku ya Sheria nchini, Kaimu jaji Mkuu wa Tanzania
Mheshimiwa Profesa Ibrahim Juma alisema Mahakama sita za Mikoa
zitajengwa ndani ya miezi 6-12 wakati Mahakama za Wilaya 19 na za Mwanzo
36 zinatarajiwa kukamilika ifikapo Desemba 2017.
Post a Comment