Na Daudi Manongi-MAELEZO.
Serikali kupitia Wizara ya
Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto imeanza hatua za awali za
uainishaji wa gharama,uandaaji wa mfumo mbadala na upembuzi wa kina wa
aina ya ubia ili kushirikiana na Sekta binafsi katika utoaji wa huduma
za uchunguzi wa magonjwa.
Hayo yamesemwa leo bungeni na
Naibu Waziri, Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wazee na Watoto
Mhe.Hamis Kigwangalla wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge Mjini
Dodoma.
“Kufuatia kukua kwa kasi kwa
Sayansi na Teknolojia ya uchunguzi wa magonjwa,Wizara inakubaliana na
wazo hili juu ya kuangalia namna nzuri ya kushirikiana na sekta binafsi
katika utoaji wa huduma hizi,”Alisema Mhe.Kigwangalla.
Amesema kwa kuanzia sasa Wizara
yake inafikiria kuanzisha ushirikiano kwa kupitia ukodishaji wa vifaa
ambapo Serikali itakodisha mashine hizo ambazo zitakuwa za mbia na
Serikali haitahusika na ununuzi,ufungaji na matengenezo kinga ya mashine
hizo.
Aidha amebainisha kuwa katika
mfumo huo,Wizara itakuwa na jukumu la kusimamia utoaji wa huduma na
itapata gawio lake kutokana na makusanyo yatokanayo na uchangiaji wa
huduma kulingana na mkataba.
“Ni imani ya Wizara kuwa kutumia
mfumo wa ubia na sekta binafsi(PPP) huduma za uchunguzi wa magonjwa
zitaimarika na kuipunguzia Serikali mzigo wa gharama”,Aliongeza
Mhe.Kigwangalla.
Post a Comment