Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,
Nyabaganga Taraba akionesha masuke ya zao la mtama wakati akikagua
mojawapo ya mashamba ya wakulima wa Kata ya Mwaweja wakati wa ziara
yake.
Mkulima wa mtama, Mariam
Nkinga (kulia) akiwaonesha Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Taraba
na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Shadrack Kangese mtama uliochanua
katika shamba lake.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,
Nyabaganga Taraba (katikati) akiangalia mtama katika shamba lililopo
kata ya Mwaweja wakati wa ziara yake.
Katibu Tawala wa Wilaya ya
Kishapu, Shadrack Kangese (kulia) na Ofisa Kilimo halmashauri ya wilaya
hiyo, Sarai Pura wakiangalia mtama uliostawi katika shamba.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu,
Nyabaganga Taraba (wa pili kulia) akibadilishana mawazo na mkulima,
Sendama Luhende, Ofisa Kilimo, Sarai Pura na mkulima Mariam Nkinga
wakati wakikagua shamba.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu akiendelea kukagua shamba la mtama katika Kata ya Mwaweja.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga akikagua shamba darasa lililolimwa na Ofisa ugani Kata ya Uchunga, Aristidia Tasingwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu mkoani
Shinyanga, Nyabaganga Taraba amewaagiza maofisa ugani wa kata zote
kuhakikisha wanawafikia wakulima na kuwafundisha mbinu bora za kilimo
chenye tija.
Ameagiza pia wananchi kulima mazao
yanayostahimili ukame hususan mtama na uwele badala ya kuwa na kasumba
ya kung’ang’ania kilimo cha mahindi ambacho katika sehemu kubwa ya
wilaya hakifanyi vizuri.
Taraba alitoa agizo hilo wakati wa
ziara yake kwenye mashamba ya mtama katika kata za Uchunga, Mwaweja na
Ukenyenge kujionea na kufanya tathmini ya kilimo wilayani humo.
Aliwataka maofisa hao kujiwekea
utamaduni wa kutembelea mashamba ili kuwafundisha namna ya matumizi ya
mbegu bora kwani wengi wao hupanda bila utaalamu.
Aliwataka kusimamia Sheria ndogo
ya mwaka 2008 ya Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu inasisitiza kuwa kila
kaya wilayani humo iweze kulima ekari mbili za mazao yanayostahili ukame
ambayo ni mtama.
Mkuu wa wilaya hiyo alisema kuwa
hata hivyo wakulima wengi wilayani humo wameweza kutekeleza sheria ndogo
hiyo lakini wamepata changamoto mbalimbali zikiwemo ukosefu wa maarifa
ya matumizi ya aina sahihi za mbegu.
“Ziara hii imetufundisha mambo
mengi kwa mfano shambani hapa tumeshuhudia wakulima hawa wametumia mbegu
za aina tano tofauti katika shamba moja sasa kama wangepata elimu
wangetumia mbegu za aina moja zisizoshambuliwa na ndege.
”Hivyo naagiza wataalamu wa kilimo
wahamie mashambani kufundisha wakulima na wawe na mashamba darasa yawe
mfano wa kujifunzia wananchi nao waige na kusonga mbele,” alisisitiza
Taraba.
Aidha, alipiga marufuku wakulima
kuuza wa mazao kwa ajili ya matumizi mengine pasipo kujiwekea akiba na
kuonya atakayefanya hivyo atachuliwa hatua kali ikiwemo kupigwa faini.
Taraba ambaye pia ni mwenyekiti wa
Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya alionya kuwa wapo baadhi ya wakulima
wana tabia ya kufanya biashara ya mtama kwa ajili ya kutengeneza pombe
huku wao wakibaki bila ya chakula.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake
mkulima wa mtama katika Kata ya Mwaweja, Mariam Nkinga kwa niaba ya
wenzake aliomba Serikali iwapelekee mbegu fupi zinazokua kwa haraka.
Alisema wanapata changamoto ya
mtama wao kuliwa na ndege aina ya kwelea pamoja na wadudu ukiwa shambani
kutokana na mbegu wanazotumia kuchelewa kukomaa na hivyo kukaa muda
mrefu shambani.
Nkinga alioimba wataalamu wawe
wanapita mara kwa mara kunyunyizia dawa mazalia ya wadudu na ndege
waharibifu wa mazao ili wasiweze kuzaliana na kufika mashambani.
Aliwashauri wananchi kulima zao la
mtama kwa wingi na kuacha kasumba ya kuchagua chakula na kulima mahindi
ambayo matokeo yake hawastawi yanakufa kutokana na ukame.
Post a Comment