Mwenyekiti wa Umoja wa Kilimo cha
Mbogamboga Wilaya ya Temeke, Joseph Kunguru (katikati) akizungumza na
waandishi wa habari kuhusu Kampeni ya kuwahamasisha Vijana kujihusisha
na kilimo cha kisasa cha Mbogamboga na Matunda leo Jijini Dar es Salaam.
Kutoka kushoto ni Diwani wa Kata ya Buza, Manispaa ya Temeke, James
Raphael Mkude na Makamu Mwenyekiti wa Umoja huo Waziri Pembe Waziri.
Diwani wa Kata ya Buza Manispaa ya
Temeke James Raphael Mkude akifafanua jambo mbele ya waandishi wa
habari kuhusiana Kampeni ya kuwahamasisha vijana kujihusisha na kilimo
cha kisasa cha Mbogamboga na Matunda leo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya waandishi wa habari
wakifatilia kwa umakini mkutano baina yao na viongozi wa Umoja wa Kilimo
cha Mbogamboga na Matunda leo Jijini Dar es Salaam.
Picha na: Husna Saidi – MAELEZO.
………….
Na Nuru Juma na Husna Saidi-MAELEZO
Umoja wa Kilimo cha Mbogamboga,
Matunda na Nafaka umeanzisha Kampeni ya Kijana Inuka na Kilimo cha
Mbogamboga na Matunda kwa lengo la kuepukana na kilimo cha mvua na
vijana waweze kujiajiri wenyewe.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa
Umoja huo Wilaya ya Temeke Joseph Kunguru alipokutana na waandishi wa
habari leo Jijini Dar es Salaam.
Kunguru alisema kuwa kilimo hicho
ni kilimo biashara na kinahitaji maji na miundombinu ya uhakika ili
kuwafanya wananchi kulima kilimo chenye tija badala ya kulima kwa
kutegemea mvua.
“Kilimo hiki kinaonekana ni kilimo
ghari sana kwani ujenzi wa Green House unaonekana ni kilimo cha watu
wenye pesa lakini ukweli ni kwamba wananchi wakiungana pamoja katika
kilimo hiki wanaweza kufanikiwa badala ya kulima kwa kutegemea mvua,”
alisema Kunguru.
Aidha alisema kuwa vijana wengi
mtaani hawana ajira hivyo viongozi kupitia kampeni hii watumie fursa
hiyo kuwaelimisha kuhusiana na kilimo hiki cha umwagiliaji ili waweze
kujiajiri wenyewe.
Umoja huo wa kilimo cha Mbogamboga
na Matunda na Nafaka umesajiliwa kisheria na ulianza na wanachama 17
mpaka sasa wapo 100 ila wanachama hai wapo 74 hivyo wanawasihi wananchi
waendelee kujitokeza kujiunga.
Kwa upande wake mmoja wa
wanakikundi hicho Sifa Karuka alisema alihamasika kujiunga na kikundi
hicho baada ya kupata taarifa kuhusu kilimo hicho cha kisasa licha ya
kuwa na shughuli zake binafsi hivyo anawasihi wakinamama na wasichana
wajitokeze kwa wingi ili waweze kujiendeleza kiuchumi.
Nae Diwani wa Kata ya Buza James
Raphael Mkude aliwahamasisha madiwani wenzie kuweza kuunda vikundi kama
hivyo katika kata zao ili wananchi wao hasa vijana wasiokuwa na ajira
waweze kujikwamua kiuchumi.
Kikundi hicho kimeiomba Serikali
kupitia Maofisa Ugani kutoa mafunzo kwa vijana ambao hawana ajira
kuhusiana nakilimo hicho ili kupunguza ukosefu wa ajira kwa kujitegemea
wao wenyewe.
Post a Comment