Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Shekhe asimamishwa baada ya kukutwa na picha chafu kwenye simu

KATIKA kile kinachoonekana ni simu ya mkononi kumponza kiongozi wa kidini, Kamati ya Mashekhe mkoani Mwanza imemsimamisha kazi kwa muda usiojulikana Shekhe wa Wilaya ya Sengerema, Ahmad Ally Jaha, kwa madai ya kukutwa na picha zisizo na staha.

Nafasi yake amekaimishwa, Shekhe Hassan Nuhu,wakati wakingoja kupatikana kwa shekhe mwingine atakayerithi mikoba ya mtangulizi wake.

Imedaiwa chanzo cha kufikia uamuzi huo ni malalamiko yaliyotolewa na mke wa shekhe huyo baada ya kumbaini mumewe anamiliki picha zisizoendana na maadili ya dini ya Kiislamu katika simu yake ya mkononi.

Picha hizo zilionekana kumsononesha zaidi kwa kuwa mumewe ni kiongozi wa dini na kwamba hakupaswa kuwa na vitu hivyo hali iliyomlazimu kupeleka malalamiko yake kwenye kamati hiyo.

Katibu wa Baraza kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Wilaya ya Sengerema, Madaraka Zubery, alilithibitishia gazeti hili wakati akizungumza na waandishi wa habari kuwa habari hizo ni kweli na kwamba baada ya uamuzi huo shekhe huyo aliitwa ili kupokea barua ya maamuzi yaliyofikiwa na uongozi.

Alisema kikao cha kamati ya mashekhe wa mkoa wa Mwanza iliyokaa Aprili 10, mwaka huu ikiongozwa na Shekhe wa mkoa wa Mwanza, Salum Fereji, ilifikia uamuzi wa kumsimamisha katika nafasi hiyo kutokana na kukiuka misingi na maadili ya Kiislamu na kutumia vibaya madaraka yake.

Aidha, baada ya barua hiyo kufika katika ofisi za Bakwata Sengerema, Kamati ya Mashekhe Wilaya ya Sengerema iliyokaa Aprili16, mwaka huu ilimteua, Shekhe Hassan Nuhu, aliyekuwa mjumbe wa kamati ya mashekhe wilaya hiyo, kukaimu nafasi hiyo wakati wakingoja taarifa iliyopelekwa makao makuu ya Bakwata taifa iwapo wataridhia kumwondoa kabisa.

Shekhe Nuhu, alipoulizwa ukweli wa yeye kukaimishwa nafasi hiyo alikiri na kuahidi kuwatumikia waumini wa dini hiyo na kuwataka waumini kusahau yaliyojitokeza ambayo yanakwenda kinyume na maadili ya Kiislamu na kila mmoja asimamie misingi ya dini na kumtukuza mwenyezi Mungu.

NIPASHE lilimtafuta kwa njia ya simu, Shekhe Ahmed Ally Jaha, kuzungumzia madai hayo na kudai hana taarifa zozote juu ya suala hilo  na sasa yuko mkoani Geita  katika mgodi wa GGM akiendelea na kazi za kujiingizia kipato.

"Ninachofahamu nilipigiwa simu na katibu wa Bakwata wilaya ya Sengerema kuwa nifike ofisini nikachukue barua yangu na niliahidi kwenda siku ya Ijumaa...hivyo nitakuwa na la kusema iwapo nitaipata na kuisoma,"alisema Shekhe Jaha.
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget