Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar
Dkt. Abdalla Juma Saadala “Mabodi” akizungumza na Wajumbe wa Baraza la
Wazee wa CCM Kisiwani humo katika Ofisi ya Kitengo cha Uratibu wa CCM
Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba.
…………………………………………………..
NA IS-HAKA OMAR, PEMBA.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM
Zanzibar, Dkt. Abdalla Juma Saadala” Mabodi” amewasihi Wazee wa Chama
hicho kisiwani Pemba kusimamia ipasavyo suala la Maadili kwa vijana ili
waishi wakiwa na uzalendo wa kweli wa kukitumikia na kukilinda chama
dhidi ya wapinga maendeleo wanaotamani kuking’oa madarakani.
Nasaha hizo amezitoa wakati
akizungumza na Baraza la Wazee wa Chama hicho kisiwani humo wakati
akihitimisha ziara yake kisiwani humo huko katika Afisi ya kitengo cha
Uratibu wa CCM, Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba .
Alisema Wazee ni hazina kubwa kwa
chama na taifa kwa ujumla kutokana na busara na nasaha zao kuwa ni
muongozo mwa nyenzo za kuongeza ufanisi wa maendeleo ya chama hicho
katika nyanja ya kisiasa na kiuchumi.
Dkt. Mabodi aliwambia Wazee hao
kwamba endapo wataweka mkakati maalum wa kukaa na vijana wao kuwaeleza
historia ya Zanzibar kabla na baada ya mapinduzi nasaha hizo
zitawajengea ukomavu na misimamo imara ya uzalendo juu ya CCM.
Pia alisema maendeleo na fursa
mbali mbali za kiuchumi zilizopo nchi kwa sasa zimetokana na utumishi
mzuri,uadilifu na uzalendo wa viongozi hao wastaafu katika sekta za
chama na serikali hivyo bado wana nafasi kubwa ya kutumia ujuzi wao
kushauri na kukosoa baadhi ya mambo wanayoona hayaendani na misingi ya
Wana ASP waliofanya Mapinduzi ya 1964.
“Katika Sayansi ya kisiasa
Wataalamu wanaamini kwamba hakuna upinzani unaodumu katika maisha ya
Serikali Tawala inayoongoza nchi kwa mfumo wa utawala wa bora, Haki, Utu
na Usawa kwa wananchi wote.
Pia Chama chetu hakina uadui na
wapinzani siku zote tumekuwa tukiwasihi watushauri na kutukosoa
watakavyo juu ya masuala mbali mbali ya kisera na Ilaya ya Uchaguzi ya
CCM ya mwaka 2015/ 2020, lakini wasiharibu wala kuchafua amani na
utulivu wa nchi yetu kwani wao jukumu lao ni siasa na sio vurugu na
migogoro hayo hatuwezi kuyavumilia”, alieleza Dkt. Mabodi.
Aidha alitoa agizo kwa viongozi
na watendaji wa Chama hicho kufanya utafti wa kitaalamu kwa baadhi ya
majimbo ya Pemba ambayo CCM imekuwa ikiaminishwa kwamba inashindwa kwa
kila uchaguzi, jambo ambalo alidai sio sahihi mpaka apate maelezo ya
kitaalamu ili kuhakikisha majimbo yote ya Pemba yanarudi mikononi mwa
chama hicho 2020.
Naibu Katibu Mkuu huyo alitamka
kuwa maandalizi ya kuandika historia mpya ya kisiasa kisiwani Pemba toka
kuasisiwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, yanaanza sasa kutokana
na kuwepo kwa mamia ya wanachama wa CUF wanaotamani kuhamia CCM wakati
wowote baada ya Chama chao kukosa muelekeo wa kisiasa na kutawaliwa na
migogoro ya wenyewe kwa wenyewe.
Alisema kwamba chama hicho
kinatambua na kulaani vitendo vya uonevu wanavyofanyiwa wafuasi wa CCM
vinavyosadikiwa kutekelezwa na wapinzani kisiwani humo ambao
wanachochewa na viongozi wao, lakini serikali kupitia vyombo vya Dola
wamekuwa wakithibiti hali hiyo, huku Chama kikitafuta ufumbuzi wa kudumu
katika kuthibiti hali hiyo.
“ Wanachama wetu wanapopigwa
kuchomewa nyumba, kung’olewa mazao yao, kuharibiwa kwa miundombinu ya
barabara na kuchomwa ofisi za umma hatusikii viongozi wa CUF wakikemea
vitendo hivyo hali ya kuwa wanaofanyiwa sio raia ama hawana haki ya
kuishi Pemba kwa Amani”, alisema CCM itaendelea kufanya siasa za
kistaarabu Zanzibar lakini haitovumilia vitendo vya uonevu wakati
yenywe ndiyo iliyoweka serikali madarani na kuvisisitiza Vyombo vya
Ulinzi na Usalama kutafuta ufumbuzi wa tatizo haraka.
Dkt. Mabodi aliwapongeza Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Dkt.John
Pombe Magufuli pamoja na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein ambaye
pia ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar, kwa juhudi zao katika
kusimamia utekelezaji wa Ilani ya CCM kwa wananchi wote bila ya ubaguzi
kwa zaidi ya asilimia 90.
Alisema Pemba kwa sasa imekuwa na
miundombinu yote muhimu ambayo zamani walikuwa wakiifuata nje ya kisiwa
hicho lakini kwa sasa imeimarishwa na Serikali inayotokana na CCM kama
ilivyoahidi kwa wananchi kuwa itatoa huduma hizo.
Nao Wazee hao walisifu juhudi za
Naibu Katibu Mkuu huyo kwa kasi yake ya utendaji unaolenga kuongeza
uimara na nguvu za CCM Zanzibar ambapo wamemtaka awakumbushe baadhi ya
viongozi wengine wafuate nyayo zake.
Hata hivyo walimpongeza Dkt.
Shein kwa juhudi zake za kuimarisha Sekta ya Afya na miundombinu ya
barabara kisiwani Pemba ambayo ni pamoja na uimarishaji wa Hospitali ya
Abdalla Mzee inayotoa huduma za kisasa, ambapo wameahidi kuthamini na
kulinda huduma hizo.
Post a Comment