Kikosi cha Mbao FC cha mkoani Mwanza kina imani ya kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho kwa kuing’oa na kuivua ubingwa Yanga.
Mbao FC wanajiamini
kutokana na safu nzuri ya ushambuliaji, lakini wameandaa safu yao ya
ulinzi kikamilifu kuwadhibiti Simon Msuva na Amissi Tambwe, kuhakikisha
hawapati nafasi ya kufunga.
Mbao inatarajia
kukutana na Yanga Jumapili katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza
katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la FA ambapo hadi sasa ni timu
nne tu ndizo zilizobakia.
Msemaji wa Mbao FC,
Chrisant Malinzi, amesema kuwa, walikuwa na hamu kubwa ya kukutana na
Yanga kwenye FA na kudai kuwa wameiandaa ipasavyo safu yao ya ulinzi
kuhakikisha wanatoa upinzani mkubwa kwa Msuva na Tambwe ili wasipate
nafasi ya kufunga kwa kuwa wanahitaji kutinga fainali.
“Tulianza mipango
yetu siku nyingi ya kujiandaa katika michuano ya Kombe la FA na tulikuwa
tukisubiria tu timu ya kupangwa nayo, tulikuwa na kiu ya kucheza na
Yanga, kwani tupo tayari kwa mchezo huo na wala hatuhofii safu ya
ushambuliaji ya Yanga kwani na sisi tuna safu nzuri ya ulinzi ya kuweza
kuwazuia Msuva na Tambwe, tumejipanga vyema kuhakikisha tunapata nafasi
ya kuingia fainali.
“Kikosi chetu kipo
vizuri na hadi tunafikia hapa ni juhudi za wachezaji hivyo nina imani
tutafanikiwa kufanya vyema na hatimaye kuingia fainali kwani lengo letu
ni kuona tunafanikiwa kutwaa taji ili kuwakilisha nchi kimataifa,”
alisema Malinzi.
Post a Comment