Kila mtanzania ametakiwa
kuhakikisha anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar ulioasisiwa miaka 53 iliyopita.
Akizungumza leo wakati akihutubia
wananchi katika sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano katika
uwanja wa Jamhuri uliopo mjini Dodoma, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli alisema kuwa ni muhimu watanzania
wakalinda Muungano kwa vile una manufaa kwa nchi zote mbili.
“Kila mtanzania ahakikishe
anafanya jitihada za kuimarisha na kulinda Muungano we
tu, kwa vile
Muungano na amani iliyopo nchini ndio chachu ya maendeleo yetu” alisema
Rais Magufuli.
Rais Magufuli alisisitiza kuwa
“Muungano ndio silaha yetu, ni nguvu yetu, mimi na mwenzangu Dkt. Shein
tutaulinda Muungano kwa nguvu zote na yeyote atakayejaribu kuuvunja
atavunjika yeye” alisema Rais Magufuli
Akitaja baadhi ya mafanikio
yaliyopatikana katika miaka 53 ya Muungano kati ya Tanganyika na
Zanzibar ni pamoja na kuunganisha mataifa mawili na kuunda taifa moja
lenye nguvu.
Rais Magufuli alitaja mafanikio
mengine ni pamoja na kuwa ni kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga,
majini, nchi kavu na reli, kukabiliana na matatizo ya umaskini, ukosefu
wa ajira na kukua kwa uhusiano wa diplomasia kati ya Tanzania na
mataifa mbalimbali ambapo yamepelekea mafanikio katika nyanja za
kiuchumi, kisiasa, na jamii.
Aidha, hii ni mara ya kwanza kwa
sherehe za Maadhimisho ya Muungano kufanyika mkoani Dodoma ambapo, Rais
Magufuli alisema kuwa Serikali imeendelea kufanya jitihada mbalimbali za
kujenga miundombinu ili kufikia azma yake ya kuhamishia makao yake
makuu mjini Dodoma ifikapo mwaka 2020.
“Niwahakikishie wana Dodoma na
Watanzania kwa ujumla kwamba Serikali sasa tumefika Dodoma na hatutarudi
nyuma tena,ambapo awamu ya kwanza ya watumishi wa Serikali takribani
3,000 kwa ngazi za Mawaziri,Naibu Waziri,Makatibu wakuu na Manaibu
Katibu wakuu wameshahamia Dodoma, kama tulivyoahidi kufikia mwaka 2020,
Serikali yote itakuwa imehamia hapa”, alisisitiza Rais Magufuli.
Sherehe za Maadhimisho ya miaka 53 ya Muungano zenye kauli mbiu isemayo “Miaka 53 ya Muungano, tuulinde na kuimarisha, tupige vita dawa za kulevya na kufanyakazi kwa bidii”,
zilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na wajane wa
viongozi waasisi wa Muungano ambapo ni Mama Maria Nyerere na Mama
Shadya Karume.
Post a Comment