WAKATI Kamati ya Katiba, Sheria na Hadhi za Wachezaji ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikitarajia kukutana kesho jijini Dar
es Salaam, uongozi wa vinara wa Ligi Kuu Bara, Simba -
wameitahadharisha kamati hiyo kutokwenda kinyume na taratibu zilizowekwa katika kufanya uamuzi kwenye ngazi mbalimbali.
Akizungumza jana, Mkuu wa Idara ya Habari na
Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema klabu yake inasisitiza kila
mwenye haki anatakiwa apatiwe kwa wakati unaofaa na kamwe si kuonyesha
viashiria vya TFF kuzipendelea baadhi ya klabu au wanachama wa
shirikisho hilo.
Manara alisema msingi wa kuheshimu vyombo vilivyopo
unatakiwa kuheshimiwa huku pia akishangaa kuona Kamati ya Katiba, Sheria
na Hadhi za Wachezaji inakutana kujadili uamuzi wa rufaa ya Simba
wakati Kagera Sugar iliandika barua ya kuomba marejeo.
"Tunaomba haki itendeke, tunatoa tahadhari kuhusiana na
kikao hicho, hatuoni uhalali wa kamati hiyo kukutana wakati Kagera Sugar
katika barua yake imeomba uamuzi uliotolewa kufanyiwa marejeo, hii
inatupa wasiwasi kuna nini hapa," alisema Manara.
Aliongeza kuwa sheria iko wazi inaeleza mtu, taasisi au
klabu inapoomba hukumu ifanyiwe marejeo, basi kesi hiyo hupelekwa katika
kamati au chombo kile kile na si vinginevyo.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Simba, Ismail Aden Rage, amewataka
viongozi wake kutokaa kimya endapo klabu hiyo itanyang'anywa pointi na
kueleza kuwa msingi wa kuheshimu kanuni na sheria ndiyo unatakiwa
kufuatwa na si matakwa au kusikiliza presha za upande wowote.
Kanuni ya bodi ya ligi namba 39 (5) (b na c) inaeleza kuwa
mamlaka yenye uamuzi wa mwisho kufanya uamuzi ni Kamati ya Katiba,
Sheria na Hadhi za Wachezaji.
Wakati huo huo ujumbe wa watu watatu wa Kagera Sugar jana
ulianza safari kuja jijini kwa ajili ya kuitika wito uliotolewa na TFF
wa kuhudhuria kikao cha Kamati ya Sheria, Katiba na Hadhi za Wachezaji
ambacho pia kitahudhuriwa na watendaji wa Bodi ya Ligi , waamuzi na
kamisaa waliochezesha mchezo huo.
Katika kikao hicho, Kagera Sugar itawakilishwa na mratibu
wa timu hiyo, Mohammed Hussein, kocha wa makipa na mchezaji Mohammed
Fakhi ambaye anadaiwa kucheza akiwa na kadi tatu za njano katika mechi
iliyoihusisha timu yake dhidi ya African Lyon.
Simba ndiyo ambayo inaongoza katika msimamo wa ligi ikiwa
na pointi 62, jana ndiyo ilipewa barua rasmi ya kuonyesha kushinda
rufani yao dhidi ya Kagera Sugar iliyotolewa na Bodi ya Ligi.
Post a Comment