NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI
MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita , jana
amezindua mashindano ya ngumi ya kombe la mstahiki Meya na kusisitiza kuwa kuna
kila sababu ya kutoa kipaumbele kwenye mchezo huo ili uweze kuwa ajira sambamba
na kuibua vipaji kwa vijana.
Meya Mwita alisema
kuwa michezo ni afya na kwamba atajitoa kadiri ya uwezo wake ili kufanikisha
mchezo huo kuwa chanzo cha ajira kama ilivyokuwa kwenye nchi za nje.
Alifafanua kuwa nchi nyingine wapo watu walioajiriwa kupitia
mchezo huo na kwamba hata hapa kwetu uwezo huo upo lakini kinachotakiwa ni
kujitoa na kuthamiria kuwekeza nguvu kubwa kwenye mchezo huo.
“ Mchezo ni afya, leo hii nimefarijika sana kuona vijana
wengi waliojitokeza kushiriki mpambano huu, kutokana na hilo kama meya wa jiji
hili, na mdhamini mkuu wa mashindao haya, nitakuwa pamoja na nyinyi” alisema
Meya Mwita.
Akizungumzia changamoto zilizotolewa na Mwenyekiti wa chama
cha ngumi mkoa wa Dar es Salaam, Carol Godfrey , Meya mwita alisema atasaidia kutoa vifaa vya michezo huku
changamoto ya uwanja akiahidi kulishughulikia.
Aliongeza kwamba kwakuwa anahitaji maendeleo ya mchezo wa
ngumi, atahakikisha kuwa kwa nafasi aliyokuwa nayo anawawezesha wachezaji ikiwa
ni lengo la kuhamasisha vijana wengi wenye vipaji vya mchezo huo kujitokeza.
“ Najua wapo vijana ambao wanavipaji wa mchezo huu, lakini
bila kuwezeshwa hatuwezi kuwapata wala kusonga mbele, sasa niweke akiba ya
maneno, lakini nitalisimamia” aliongeza.
Akizungumzia mashindano
hayo, Meya Mwita alisema kuwa waamuzi wa mchezo huo (Marefa) wanapaswa kutenda
haki bila kuwepo hali ya hujuma na kwamba anayestahili kupata tuzo hiyo ndio
apatiwe.
Alisema wapo baadhi ya waamuzi wa michezo mbalimbali sio
waminifu na kwamba wamekuwa na tabia ya kupanga matokeo , hivyo akaonya kwa kusisitiza
kuwa jambo hilo kwenye mashinda hayo lisijitokeze.
“ Waamuzi naomba muwe waminifu, ili muweze kujenga imani kwa
watu ambao mko nao hapa, jambo la kupanga matokeo sio zuri, hivyo aliyestahili
kushinda ndio apewe nafasi hiyo nasio kupindisha matokeo” alisema Meya Mwita.
Hata hivyo katika hatua nyingine aliwataka wachezaji wote
walioshiriki michuano hiyo, kuzingatia sheria na kuwaheshimu walimu
wanaowafundisha ili kujenga nidhamu bora ya mchezo huo.
Post a Comment