Serikali imeitaka Bodi ya Chuo Cha
Bahari Dar es Salaam (DMI), kuhakikisha inaboresha miundombinu ya chuo
na kuzingatia miiko na kanuni za ufundishaji ili wanafunzi wanaohitimu
chuoni hapo waweze kukidhi mahitaji ya soko.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, amesema hayo leo jijini Dar es
salaam, wakati akizindua bodi hiyo na kusisitiza kuweka mikakati
madhubuti ya kuboresha majengo kwa kutangaza zabuni kwa uwazi ili
kuepuka mianya ya rushwa.
“Hakikisheni mnakuwa na mpango
madubuti wa kuboresha majengo ya chuo ili chuo kibaki na hadhi yake,
lakini pia hakikisheni mntoa elimu bora kwa wanafunzi wanaokuja kusoma
hapa ili waweze kupata misingi imara itakayowawezesha kuajiriwa ndani
na nje ya nchi mara baada ya kuhitimu masomo yao”, amesema Waziri Prof.
Mbarawa.
Ameongeza kuwa Serikali ina
uhitaji wa wataalam wengi kwenye masuala ya bahari hivyo ni wajibu wa
bodi kusimamia chuo na kuhakikisha wataalam hao wanazalishwa kwa wingi
chuoni hapo ili kukidhi mahitaji ya soko kitaifa na kimataifa.
Amewataka wakufunzi wa chuo hicho
kuhakikisha wanatumia lugha nzuri kwenye ufundishaji ili kuwaweka
wanafunzi karibu na kuhakikisha wanapata taaluma inayotakiwa kwani
kuwepo kwa waalimu hao kunategemea kuwepo kwa wanafunzi.
“Ni lazima tufungue milango kwa
wanafunzi sababu wapo wanaoelewa haraka na wanaoelewa taratibu, hivyo
tukae nao muda mrefu ili kubaini changamoto zao lakini pia tuwe
waangalifu juu ya matumizi ya lugha tunazotumia kwa wanafunzi wakati
tunapofundisha”, amefafanua Prof. Mbarawa.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mpya wa
Bodi ya DMI, Kapteni Ernest Bupamba, amemuahidi Waziri huyo kuwa
watafanya kazi ya kusimamia chuo hicho kwa juhudi zote na kwa maarifa
yote ili chuo kizalishe wataalam wenye sifa kwenye sekta ya uchukuzi,
“Naahidi kushirikiana vyema na
Wajumbe wezangu wa bodi, Menejimenti ya Chuo na watumishi katika
utekelezaji wa majukumu ili kuleta tija’ amesisitiza Kapteni Bupamba.
Aidha, Mkuu wa Chuo hicho Dkt.
Erick Massami amemuomba Waziri Mbarawa kukisaidia chuo hicho kuanza
kutumia fedha za mfuko wa Usafirishaji ambazo zimekusanywa tangu mwaka
2013 bila kutumika ili fedha hizo zitumike kuzalisha wataalam wengi
katika sekta ya usafiri wa majini.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua bodi ya chuo ambayo iko
chini ya uenyekiti wa Kapteni Ernest Bupamba na wajumbe wanne ambao ni
Kapteni Andrew Matilya, Dkt. Mwamini Tulli, Bi Tumaini Silaa na Eng.
Alfred Waryana.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Post a Comment