Kiongozi wa timu ya mpira wa
kikapu ya Weusi Basketball Club ya jijini Dar es Salaam, Mntambo Mngeja
(kulia) akipata maelekezo ya juu ya kujiandikisha kutoka kwa mratibu ya
michuano ya Sprite Bball Kings, Basilisa Biseko wakati wa zoezi la
uandikishaji wa timu mbalimbali kwa ajili ya ushiriki wa michuano hiyo.
Uandikishaji ulifanyika Tegeta Complex jijini Dar es Salaam huku timu
zaidi ya 20 zikijitokeza kujiandikisha. Michuani ya Sprite Bball Kings
inaendeshwa na kituo cha Televisheni na Radio cha East Africa
(EATV/Radio) kwa udhamini wakampuni ya Coca-Cola.
Na Mwandishi Wetu, Dar.
Ikiwa ni siku ya kwanza kwa timu
mbali mbali za michuani ya kikapu ya Bball Kings, zaidi ya timu 20
zimejitokeza kujiandikisha mwishoni mwa wiki hii wakati wa zoezi la
uandikishaji linaloendelea jijini Dar es Salaam.
Michuani ya mchezo wa kikapu ya
Bball Kings inayoendeshwa na kituo cha Televisheni na Radio cha East
Africa (EATV/Radio) kwa kushirikiana na Kampuni ya Coca-Cola kupitia
kinywaji chake cha Sprite siku ya jumamosi imeshuhudia wawakilishi wa
timu mbalimbali wakijitokeza na kujaza fomu za ushiriki, huku
wawakilishi wa timu hizo wakijigamba kujidhatiti kikamilifu kuchukua
ubingwa wa mwaka huu.
Kati ya timu zilizojitokeza ni pamoja na Cavarious, Lycans, Tegeta Camp, Lord Baden, K-Warriors, DMI, St Joseph na MJ Junior.
Nyingine ni Oilers, TMT, Mchenga,
Bahari Beach, Street Boys, Street Warriors, Chanika Legends, God With
Us, Weusi Basketball Club, Junior Basketball Club na Celestial
Basketball Team.
Akizungumza wakati wa uandikishaji
wa timu shiriki, Mkuu wa Kitengo cha Mauzo na Masoko wa wa EATV, Roy
Mbowe alisema mwitikio wa timu mbalimbali umejaa hamasa kubwa na wa
kuridhisha, huku kila timu iliyojitokeza ikiwa na wachezaji wasiozidi
10.
“Mashindano hayo yanahusu vijana
wenye umri wa kuanzia miaka 16 na watapaswa kuunda timu ya wachezaji 10
ambao watachuana na timu nyingine zitakazokuwa zimejiandikisha, huku
tukitoa fursa katika wachezaji hao 10, timu inaweza kuwa na wachezaji
wasiozidi watatu kutoka katika timu kubwa za Ligi Darasa la Kwanza za za
kikapu za hapa nchini,’’alisema Mbowe.
Michuano ya Sprite Bball Kings
itaendeshwa kwa njia ya mtoano katika hatua ya kwanza ili kupata timu 16
zitakazoingia hatua ya pili na kutaja zawadi kwa timu itakayotwaa
ubingwa itakuwa ni Sh.milioni 10 wakati mshindi wa pili atapata
Sh.milioni tatu huku pia kukiwa na zawadi ya Sh milioni mbili kwa
mchezaji bora (MVP).
Mashindano hayo yatakayoshirikisha
wachezaji kutoka mikoa yote nchini, yanatarajiwa kuanza mwezi huu na
kumalizika Julai mwanzoni.
Post a Comment