Na Tiganya Vincent, Tabora
Waziri
wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amevitaka vikundi
vyote vilivyopewa leseni ya kuanza uchimbaji mdogo mdogo wa madini ya
dhahabu katika eneo la Kitunda wilayani Sikonge kuhakikisha vinatoa
ajira kwa wachimbaji 3000 walipo katika eneo hilo.
Waziri
ametoa agizo hilo jana wilayani Sikonge katika eneo la Kitunda ,wakati
yeye na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Tabora alipotembelea
eneo lililosababisha vifo vya wachimbaji saba wa madini kwa ajili ya
kujionea na kutoa pole kwa wananchi wa eneo hilo.
Alisema
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
iliahidi wakati ikiomba kura kwa wananchi ya kuwashika mkono wachimbaji
wadogo wadogo na kwa kuwa neema hiyo imepatikana hapo ni vema vijana
wengi wa eneo hilo wenye nia ya kushiriki katika uchimbaji wa madini
wakanufaika na ajira.
Hivyo
,Profesa Muhongo alisema kuwa ni vema kila Kikundi kilichopewa leseni
na kibali cha kuanza uchimbaji mdogo mdogo kikaandaa orodha ya majina ya
vijana ambayo kitawaajiri katika mgodi wao ili Serikali ijue na iwe na
idadi kamili wanaofanyakazi katika eneo lao na kwa ajili ya usalama.
“Kila
mgodi uwe na majina ya watu wanaotaka kuwaajiri na orodha hiyo ifike
kwa Mkuu wa Mkoa , Maafisa wa Madini wa Kanda ikiwa imeonyesha jina la
kila moja na idadi yao…hatuwezi kuwacha vijana hawa wote bila
ajira”alisisitiza Waziri huyo.
Kufuatia
hatua hiyo alimuomba Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bw. Aggrey Mwanri na timu
yake kuhakikisha wanasimamia zoezi la orodheshaji wachimbaji wote
waliopo katika eneo hilo na kuwagawa katika vikundi vya Kapumpa, Winima,
Gold Stone na Mawina kwa lengo la kuhakikisha kuwa kila mtu anapata
sehemu ya kufanyia kazi na anafanyakazi katika eneo salama.
Hatua
hiyo inalenga kuondoa tabia za baadhi ya wachimbaji hao kuvamia maeneo
ya wengine na hivyo kuhatarisha maisha yao nay a wengine.
Alitoa
agalizo watu wote wanaomiliki leseni , wachimbaji na wataosimamia zoezi
hilo kuhakikisha hakuna jina litakalojitokeza katika kundi zaidi ya
moja na kuongeza kuwa ni vema mtu akafanyakazi katika kundi moja.
Profesa Muhongo alisema kuwa kuhusu suala la malipo ni juu yao kufuatia taratibu watakazojiwekea.
Katika
hatua nyingine Waziri huyo ametoa siku tatu kwa Maafisa wa Madini wa
Kanda kuhakikisha wanakamilisha haraka taratibu zinatakiwa iwemo kuwa
watu wa mazingira, upimaji wa mashimo kwa umbali unaotakiwa na upangaji
wa wachimbaji hao kulingana na vikundi vinne vilivyopewa leseni katika
eneo hilo.
Alisema
kuwa baada ya hapo Mkaguzi Mkuu wa Madini atapitia na kuona kama
taratibu zote za usalama zimezingatiwa katika eneo hilo na ndipo
Serikali itakaporuhusu zoezi hilo kuanza tena uchimbaji wa dhahabu
katika machimbo hayo.
Kwa
upande wa wachimbaji wadogo wadogo katika eneo hilo wamemuomba Waziri
huyo kuharakisha kuwaondolea zuio la kuchimba madini kwa kuwa
walitegemea kazi hiyo kama chanzo cha mapato kwa ajili ya matumizi yao
na familia zao.
Walisema kuwa kwa kipindi ambacho wamekuwa hawachimbi wamekuwa na maisha magumu kwa sababu hawana chanzo kingine cha mapato.
Wakati
huo huo wachimbaji hao wamemuhakikishia Waziri wa Nishati na Madini
Profesa Muhongo kuwa ni watu saba tu ndio waliofariki katika eneo hilo
na sivyo zaidi ya hao.
Walitoa
ufafanuzi kuwa watano walikufa pale pale kwa kufikiwa na kifusi katika
eneo linalomikiwa na moja alifariki wakati akiendelea na matibabu
hospitali na mwingine alifariki kwa kukosa hewa.
Kwa
upande wa Kamishna Msaidizi wa Madini Kanda Kati Magharibi Salim Salim
alisema kuwa ili kuhakikisha maafa mengine hayatokei, kabla ya kuanza
tena uchimbaji katika eneo hilo Ofisi ya Kanda kwa kushirikiana na Afisa
Mkazi wa Madini wameshaanza kusimamia zoezi la kuhakikisha mashimo ya
uchimbaji wa dhahabu yanakuwa wa kuanzia mita 15 toka moja kwenda
jingine.
Bw.
Salim aliongeza kuwa hatua nyingine ni kuhakikisha kuwa kila kiwanja
cha uchimbaji kina kuwa na Meneja wa kusimamia Mgodi ambaye atapanga
msimamizi wa kila shimo.
Post a Comment