Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipitia taarifa ya Mradi wa Ujenzi
wa barabara ya Mafinga –Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 Mkoani
Iringa mara baada ya kukagu mradi huo kulia ni Meneja Mradi huo Richarad
Guo akisisitiza jambo.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani akipata maelezo kutoka kwa Meneja
Mradi wa ujenzi wa barabara ya Mafinga –Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo
KM 74.1 Richarad Guo alipokagua ujenzi huo Mkoani Iringa.
Muonekano wa barabara ya Mafinga
–Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 ambapo tayari Kilomita 18
zimekamilika kwa kiwango cha lami, ujenzi huo unafanywa na kampuni ya
China Civil Engenering Construction Corporation (CCECC).
Mafundi wanaojenga barabara ya
Mafinga-Igawa sehemu ya Mafinga –Nyigo KM 74.1 Mkoani Iringa
wakiendelea na ujenzi wa karavati kubwa katika eneo chepechepe maarufu
Majinja wilayani Mufindi.
Muonekano wa Mtambo wa kusaga kokoto pamoja na shehena ya kokoto zinazotumika katika ujenzi wa barabara ya Mafinga –Igawa.
…………………………………………………………………………..
Naibu Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi
na Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amemtaka mkandarasi China Civil
Engeneer Construction Cooporation (CCECC), anayejenga barabara ya
Mafinga-Nyigo km 74.1 na (CRSG) anayejenga sehemu ya Nyigo –Igawa KM
63.8 kuongeza kasi ya ujenzi ili upanuzi na uimarishaji wa barabara
hiyo ukamilike kwa wakati.
Akizungumza mara baada ya kukagua
ujenzi huo Eng. Ngonyani amemtaka Meneja wa Wakala wa Barabara
(TANROADS) Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole kuhakikisha upana wa
barabara hiyo na ubora wake unakidhi malengo ya Serikali ili barabara
hiyo ili idumu kwa muda mrefu na kupunguza msongamano na ajali
zinazoepukika.
“Barabara hii ambayo ni sehemu ya
barabara kuu ya TANZAM inaunganisha bandari ya Dar es Salaam na nchi za
Zambia na Malawi ni muhimu sana kwa uchumi wa nchi hivyo ni lazima
isimamiwe kikamilifu ili idumu kwa muda mrefu”, amesisitiza Eng.
Ngonyani.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa
barabara hiyo Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa Eng. Daniel Kindole
amesema tayari kilomita 18 kati ya 74.1 katika sehemu ya kwanza ya
Mafinga –Nyigo imeshawekwa lami na Mkandarasi ameunda timu tatu ili
kuharakisha ujenzi huo.
“Ujenzi wa barabara ya Mafinga
-Igawa unahusisha mikoa mitatu ambapo Kilomita 74.1 ziko katika mkoa wa
Iringa Mafinga-Nyigo, Kilomita 52 ziko katika mkoa wa Njombe
Nyigo-Halali na Kilomita 12 ziko katika Mkoa wa Mbeya Halali-Igawa hivyo
mimi pamoja na wenzangu tumejipanga kuhakikisha barabara hii
inakamilika Novemba mwakani kama ilivyopangwa”, amesisitiza Eng.
Kindole.
Naye Meneja Mradi wa ujenzi wa
barabara hiyo Sehemu ya Mafinga – Nyigo KM 74.1 Richard Guo
amemhakikishia Naibu Waziri huyo kwamba kasi yao ya ujenzi ni nzuri na
barabara hiyo imeimarishwa ili kukidhi mahitaji na itakamilika kwa
wakati.
Zaidi ya shilingi bilioni 116
zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa barabara hiyo sehemu ya kwanza
yaani Mafinga- Nyigo km 74.1 ambazo zinagharamiwa na Serikali ya
Tanzania na Benki ya Dunia.
Post a Comment