Kampuni
ya Techno Net Scientific inayojishughulisha na uingizaji pamoja na
uuzaji wa kemikali imekutwa na kemikali zilizoingizwa nchini kwa njia za
udanganyifu kwa kutumia vibali vya bandia.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Mkemia Mkuu wa Serikali (GCLA),
Prof. Samwel Manyele alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu kampuni hiyo kukutwa na kemikali bashirifu bila kuwa na usajili
wala kibali cha kufanya shughuli za kuuza na kusambaza bidhaa hiyo.
Prof.
Manyele amesema kampuni hiyo ilikuwa na usajili wa miaka miwili kuanzia
April 30 mwaka 2014 hadi Aprili 30, 2016 ambapo kwa mujibu wa Sheria ya
Kemikali kampuni hiyo ilipaswa kusitisha shughuli zake hadi pale cheti
cha usajili kitakapopatikana.
“Ingawa
shughuli zake zilisitishwa lakini kampuni hiyo iliendelea kufanya kazi
bila kuwa na cheti cha usajili hivyo ofisi yangu iliungana na Mamlaka ya
Kudhibiti dawa za kulevya na Mamlaka ya Chakula na Dawa kufanya ukaguzi
wa pamoja ambapo kwa sasa tumewaachia vyombo vya dola kufanya uchunguzi
wao” amesema Prof Manyele.
Amefafanua
kuwa Sheria ya Kemikali za Viwandani na Majumbani Sura ya 182 na kanuni
zake inatoa masharti kuwa kila mtu anayetaka kujihusisha na shughuli za
kemikali kwa namna yoyote ni sharti awe amesajiliwa na kufanyiwa
ukaguzi.
Aidha,
ametoa rai kwa wafanyabiashara wote wa kemikali na umma kwa ujumla kuwa
Serikali haitasita kuchukua hatua za kisheria kwa makampuni na
wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu na wanaovunja matakwa ya Sheria
katika uingizaji, usafirishaji, uhifadhi na utumiaji wa kemikali ikiwemo
kemikali bashirifu nchini.
Prof.
Manyele amewaomba wananchi kutoa taarifa na kuwafichua wafanyabiashara
wa kemikali wanaokiuka matakwa ya Sheria kwa ajili ya kuchukuliwa hatua
stahiki za kisheria ambazo zitapelekea wengine kuwa na matumizi salama
ya kemikali na kuzuia madhara kwa watu na mazingira.
Post a Comment