Kamati ya Bodi ya Uendeshaji na
Kusimamia Ligi (Kamati ya Saa 72), iliketi mwishoni mwa wiki iliyopita
na kupitia mchezo mmoja baada ya mwingine na kuibuka na uamuzi ufuatao.
Mechi namba 212 (Yanga 2 Vs
Kagera Sugar 1). Kamati imefuta kadi nyekundu ya moja kwa moja aliyopewa
mchezaji Mbaraka Yusuf wa Kagera Sugar baada ya kubaini hakutenda kosa
lililosababisha mwamuzi ampe adhabu hiyo. Uamuzi huo umefanywa kwa
mujibu wa Kanuni ya 9(8) ya Ligi Kuu.
Pia Mwamuzi wa mechi hiyo, Ngole
Mwangole ameondolewa kuchezesha Ligi Kuu ya Vodacom kwa vile uamuzi
aliofanya haukuwa sahihi. Hatua dhidi ya Mwamuzi Mwangole imechukuliwa
kwa kuzingatia Kanuni ya 38(1a) ya Ligi Kuu.
Hii ni mara ya pili kwa Ngole
kushindwa kutafsiri sheria uwanjani kwani katika duru la kwanza alionywa
baada ya kukataa bao JKT Ruvu ilipocheza na Mtibwa Sugar katika Ligi
Kuu ya ismu huu wa 2016/17.
Mechi namba 214 (JKT Ruvu 2 Vs
Azam 2). Klabu ya Azam FC imepigwa faini ya sh. 500,000 (laki tano) kwa
kosa la kutoingia vyumbani, na badala yake kukaa nje. Kitendo hicho ni
kwenda kinyume na Kanuni ya 14(13) ya Ligi Kuu, na adhabu imetolewa kwa
mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
Mechi namba 215 (Mbao FC 1 Vs
Tanzania Prisons 0). Mchezaji Jeremiah Juma wa Tanzania Prisons
amefungiwa mechi tatu na kupigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na
kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumpiga ngumi mpinzani wake. Adhabu
hiyo imetolewa kwa mujibu wa Kanuni ya 37(3) ya Ligi Kuu.
Pia timu ya Tanzania Prisons
imeagizwa kurudisha mpira uliochukuliwa na mshabiki wake baada ya
kumalizika mechi hiyo iliyofanyika Aprili 16, 2017 kwenye Uwanja wa
Nyamagana jijini Mwanza.
Msimamizi Msaidizi wa Kituo cha
Mwanza aliripoti kwa Meneja wa Prisons, Bw. Enock Mwanguku tukio la
shabiki huyo aliyechukua mpira huo na kuingia kwenye gari la timu hiyo.
Meneja huyo aliahidi kufuatilia, lakini hadi timu yake inaondoka
uwanjani hakutoa mrejesho wowote.
Mechi namba 220 (Majimaji 3 Vs
Mwadui 0). Klabu ya Majimaji imepigwa faini ya sh. 500,000 kutokana na
timu yake kuingia uwanjani kwa kutumia mlango usio rasmi. Adhabu hiyo ni
kwa mujibu wa Kanuni ya 14(48) ya Ligi Kuu.
Mechi namba 224 (Yanga 2 Vs
Tanzania Prisons 0). Klabu zote zimepigwa faini ya sh. 500,000 kila moja
kwa timu zao kutoingia vyumbani na kusababisha wachezaji wakaguliwe
wakiwa nje ya vyumba. Adhabu hiyo ni uzingativu wa Kanuni ya 14(48) ya
Ligi Kuu.
Post a Comment