Na Jacquiline Mrisho.
Tanzania ya viwanda inayoelekea
kwenye uchumi wa kati ni moja kati ya mipango mikubwa ya Serikali ya
awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika azma yake
ya kuleta Maendeleo nchini.
Akihutubia Bunge la 11 la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania kwa mara ya kwanza baada ya kuapishwa kuwa Rais
wa awamu ya Tano, Magufuli alisema kwamba Serikali yake itaweka mkazo
mkubwa katika ujenzi wa Viwanda.
“Natambua kwamba sekta binafsi
ndiyo mhimili mkubwa wa kujenga uchumi wa viwanda. Tamaa yangu na kwa
kweli jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano zitakuwa katika ujenzi wa
uchumi wa kipato cha kati ambapo sura na maisha ya Watanzania walio
wengi yafanane na nchi za kipato cha kati” alisema Rais Magufuli.
Aidha katika hotuba hiyo Mhe.
Magufuli aliongeza kuwa ifikapo mwaka 2020 idadi ya ajira itokanayo na
viwanda imepangwa ifikie asilimia 40 ya ajira zote zitakazokuwepo nchini
wakati huo.
Serikali pekee haitaweza
kuyafikia malengo hayo bila kuwa na ushirikiano wa Wananchi pamoja na
wafanyabiashara mbalimbali kutoka sekta binafsi hivyo kwa kutambua hilo,
Sekta binafsi zimekubaliana kushiriki katika ujenzi wa viwanda.
Makubaliano hayo yalitangazwa
rasmi mbele ya Rais Dkt. Magufuli kwenye kikao cha kumi cha Baraza la
Taifa la Biashara (TPSF) kilichofanyika hivi karibuni Jijini Dar es
Salaam ambapo viongozi wa Baraza hilo walisema kuwa wameamua kwa moyo
mmoja kusaidiana na Serikali katika kutekeleza azma hiyo ya kuifanya
Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda.
Katika ripoti ya Sekta binafsi
iliyokabidhiwa kwa Mhe. Rais Magufuli ilieleza kuwa “Katika kuunga
mkono jitihada za dhati za Rais, sekta binafsi ya Tanzania imependekeza
agenda kuu ya Baraza hilo kuwa ni ‘Ushirikiano wa Sekta Binafsi na
Serikali kuelekea Uchumi wa Viwanda’.
Kama inavyofahamika duniani
kote sekta binafsi ndio muhimili mkubwa wa ukuaji wa uchumi wa taifa
lolote,hivyo ni jukumu la Serikali kuweka mazingira wezeshi kama
inavyofanya Serikali ya Awamu ya Tano ili kuvutia wawekezaji wa ndani na
nje ya nchi.
Juhudi za makusudi
zimeonyeshwa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha sekta
binafsi inawezeshwa, mfano katika ziara ya Rais wa Uturuki Mh. Recep
Tayyip Erdogan aliyoifanya hivi karibuni, wafanyabiashara zaidi ya 600
walioambatana naye walikutanishwa na sekta binafsi hapa nchini na
kubadilishana mawazo pamoja na uzoefu katika biashara.
Kadhalika alipokuja Waziri
Mkuu wa India Mh. Narendra Modi aliambatana pia na wafanyabiashara ambao
kwa umoja wao walikubaliana na sekta binafsi jinsi ya kushirikiana
katika kukuza uchumi wa viwanda hasa kuendeleza viwanda vidogo.
Aidha hivi karibuni Tanzania
ilitembelewa na Rais wa Afrika Kusini Mh. Jacob Zuma akiambatana na
Mawaziri 6 akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara Dkt. Rob Davies na
wafanyabiashara 80 ambao waliungana na wafanyabiashara wa Tanzania
kujadili mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya sekta hiyo.
Mchango mkubwa wa Serikali
pamoja na sekta binafsi chini ya uratibu wa TPSF ni wa kuigwa na wa
mfano, uzalendo waliouonyesha utaleta maendeleo hasa katika kipindi hiki
cha kuelekea uchumi wa Kati unaoshamirishwa na ujenzi wa viwanda.
Kwa mujibu wa taarifa za
TPSF,Sekta Binafsi inalenga kukuza pato la taifa kufikia asilimia 60
pamoja na kutoa asilimia 40 ya ajira kwa watanzania.
Hatuna budi kuwapongeza
wafanyabiashara na Sekta Binafsi kwa ujumla kwa kukubali kwa moyo mmoja
kushirikiana na Serikali katika kusukuma gurudumu la kuiwezesha Tanzania
kuwa nchi ya Viwanda.
Hongera TPSF, hongera Serikali kwa kuonyesha njia, ama kwa hakika mabadiliko yanakuja na Tanzania yenye neema inakaribia.
Post a Comment