Huku Bingwa wa
Ligi Kuu Bara akitarajiwa kupatikana leo, Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB)
imeandaa makombe mawili kwa ajili ya kumkabidhi bingwa, moja lipo Dar es
Salaam na lingine lipo Mwanza.
Kombe moja leo
litakuwepo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambapo Simba inacheza
na Mwadui FC ya Shinyanga na lingine litakuwa Mwanza kwenye Uwanja wa
CCM Kirumba ambapo Yanga inacheza na Mbao FC.
Yanga na Simba zote
zinawania ubingwa lakini Yanga ndiyo yenye nafasi kubwa ya kutwaa
ubingwa rasmi kwani ina pointi 68 kileleni wakati Simba ni ya pili ikiwa
na pointi 65.
Ili Yanga iwe bingwa
inahitaji sare hata kufungwa idadi ndogo ya mabao, wakati Simba
itahitaji ushindi wa mabao 12-0 huku ikiiombea Yanga kipigo.
Mkurugenzi Mtendaji
wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura amesema wameandaa makombe mawili moja
litakuwepo Uwanja wa Taifa na lingine CCM Kirumba, Mwanza.
“Tumejiandaa kuhakikisha bingwa atakayepatikana kesho (leo) anakabidhiwa kombe lake mara baada ya mechi kumalizika.
“Bado bingwa
hajajulikana kati ya Simba na Yanga na mechi zao za mwisho wanacheza
kwenye viwanja tofauti, hivyo ni lazima tuandae makombe mawili.
“Hivyo, tayari
tumeyaandaa makombe mawili kati ya hayo moja tutalikabidhi kwa bingwa
atakayelichukua kati ya Simba na Yanga,” alisema Wambura bila ya kutaka
kufafanua kuhusu utaratibu huo.
Post a Comment