Na Nuru Juma & Husna Saidi
Serikali kupitia Wizara ya Maji na
Umwagiliaji inaendelea na kutekeleza miradi mbalimbali ya maji Mijini
na Vijijini ili kuhakikisha Taifa linaondokana na kero itokanayo na
maji.
Hayo yamesemwa leo Bungeni Mjini
Dodoma na Waziri wa Maji na Umwagiliaji Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa
akijibu swali la Mhe, Leah Jeremiah Komanya Mbunge wa viti Maalum.
Mhandisi Lwenge alisema katika
kuhakikisha miradi hiyo inanufaisha jamii kama ilivyokusudiwa Wizara
yake imeandaa na inatekeleza uundaji, usajili wa vyombo vya watumiaji
maji (COWSOs) na kuzijengea uwezo kwaajili ya uendeshaji na usimamizi.
“Pamoja na utekelezaji huo
kumekuwa na changamoto mbalimbali katika miradi hiyo ikiwemo uchakavu wa
miundombinu ya maji, wizi wa vifaa vya maji pamoja na watumiaji maji
kutolipa huduma hiyo zikiwemo taasisi za Serikali hali hiyo imepelekea
mamlaka nyingi kushindwa kugharamia matengenezo ya miundombinu ya maji”
alisema Mhandisi Lwenge.
Aliongeza kuwa ili kukabiliana na
wizi wa maji pamoja na uchakavu wa miundombinu Wizara inaendelea
kurekebisha Sheria za maji ili ziweze kutoa adhabu kali kwa wezi wa maji
na wahujumu wa miundombinu ya maji.
Aidha alisema kuwa katika
kuhakikisha mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira zinatoa huduma
endelevu mamlaka hizo zinasimamiwa na bodi ambazo zinajumuisha wadau
mbalimbali.
Kwa upande mwingine alisema
mamlaka za maji safi na usafi wa mazingira mijini zinaendelea
kukarabati miundombinu ya maji iliyochakaa, kufunga dira za maji kwa
wateja wote ili kubaini matumizi yao halisi na kutoa elimu kwa jamii
kuhusu umuhimu wa kulinda miundombinu ya maji.
Aidha Wizara imeanza kuchukua
hatua za kutumia nishati ya jua kwenye mitambo ya maji hususani vijijini
kwaajili ya kupunguza gharama za uendeshaji.
Post a Comment