THE CIVIC UNITED FRONT
(CUF–Chama Cha Wananchi)
TAARIFA KWA UMMA NA VYOMBO VYA HABARI
Imetolewa leo Tarehe 15/5/2017
TAARIFA ZA CHAMA KWA WIKI CHACHE ZILIZOPITA MPAKA 14 MAY, 2017
Hii
ni wiki ya saba (15) sasa kukuletea mukhtasari wa taarifa muhimu za
Chama juu ya masuala mbalimbali kwa lengo la kuwajulisha wanachama,
viongozi na watanzania kwa ujumla yanayoendelea ndani ya CUF na kuwekana
sawia kwa kuwapa hali taarifa (Updates) na aidha kusahihisha taarifa za
upotoshwaji, hujuma na au propaganda chafu dhidi ya Chama.
KURUGENZI YA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA WIKI HII INAWAJULISHA TAARIFA ZIFUATAZO:-
1. (A) KATIBU MKUU, MAALIM SEIF KUWATEMBELEA WAZEE WAASISI WA
CUF, KUWAJULIA HALI WAGONJWA NA KUWAFARIJI WAFIWA
KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM:
Katibu
Mkuu,Maalim Seif Sharif Hamad, amewatembelea na kuwajulia hali wazee
waasisi wa CUF, wagonjwa na kuwafariji wafiwa mbalimbali katika Jiji la
Dar es Salaam. Maalim Seif amepata mapokezi makubwa na ya heshima kila
alipofika. Wananchi na Wanachama wengi wamekuwa na hamu kubwa ya
kufikiwa na ziara hiyo na kila mmoja kutaka afike katika Kata na au Tawi
lake la Chama. katika ziara hiyo Maalim Seif aliambatana na Wakurugenzi
wa Chama Taifa, Wajumbe wa Baraza Kuu. Wabunge –CUF na Manaibu Meya wa
Dar es Salaam. Katibu Mkuu ataanza ziara ya ukaguzi wa Uhai na Shughuli
mbalimbali za Chama katika Mkoa wa Dar es Salaam hivi karibuni.
(B)KATIBU MKUU KUMTEMBELEA ASKOFU GWAJIMA:
Tarehe
10/5/2017 Maalim Seif alimtembelea Askofu Josephat Gwajima Ofisini
kwake Ubungo- Dar es Salaam kumjulia hali na kubadilishana nae mawazo
juu ya masuala mbalimbali nchini. Baadae walipata fursa ya kuzungumza na
waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari nchini ambapo walieleza kuwa
wao ni marafiki na wamekutana kubadilishana mawazo.
2. MWENYEKITI WA KAMATI YA UONGOZI TAIFA MHE.JULIUS MTATIRO AFANYA ZIARA TANGA MJINI:
Mheshimiwa
Julius Mtatiro amefanya ziara ya kichama na kufanya kikao na Kamati ya
Utendaji ya Wilaya ya Tanga. Ziara hiyo ilisitishwa na Jeshi la Polisi
kwa kisingizio eti cha uvunjifu wa amani kutokana na sababu za
kiintelijensia. Pamoja na awali Jeshi hilo kupokea taarifa ya ziara hiyo
na kuruhusu kufanyika. Ghafla siku ya ziara hiyo OCD-Tanga aliandika
barua ya kusitisha ziara hiyo, pamoja na kufanya nae mazungumzo na
kujenga hoja ambazo alishindwa kuzijibu aliendelea na msimamo huo kwa
maelekezo kuwa amepata maagizo kutoka ngazi za juu. Awali Jeshi hilo na
uongozi wa Mkoa lilitaka kuwatumia kuwagawa madiwani wa CUF na viongozi
wa CUF ionekane kuwa kuna tofauti miongoni mwao ili wapate sababu lakini
hawakuweza kwani viongozi wote wa Tanga walikuwa kitu kimoja Kumpokea
Mwenyekiti wao Taifa Mhe. Julius Mtatiro.
3. TAARIFA YA KESI ZA CHAMA NAHATUA ZA KISHERIA JUU YA UVAMIZI WA WAFUASI WA LIPUMBA VINA HOTEL, MABIBO DAR ES SALAAM:-
a) Shauri la msingi namba
23/2016 lililopo kwa Jaji Kihiyo dhidi ya Msajili Jaji Francis Mutungi,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lipumba na wenzake limepangwa kutajwa
tena Tarehe 18/5/2017.
b) Mashauri
yote yanayohusiana na wizi wa fedha za Ruzuku yamepangwa kusikilizwa
Tarehe 6/6/2017 Kesi zote kwa ujumla zinaendelea na kusimamiwa vizuri
na mawakili wetu.
c) Suala
la Uvamizi wa wafuasi wa Lipumba Vina Hotel na kuwajeruhi waandishi wa
Habari na viongozi wa CUF katika Mkutano ulioitishwa na Mwenyekiti wa
Wilaya ya Kinondoni Mhe. Juma Mkumbi bado lipo mikononi mwa Kamishna wa
Polisi Kanda ya Dar es Salaam Mhe Simon Sirro. Mpaka sasa watuhumiwa
hawajafikishwa Mahakamani.
4. KAZI ZA MANAIBU MEYA WA DAR ES SALAAM MHE. MUSA KAFANA (JIJI), MHE. OMARI KUMBILAMOTO NA MHE. RAMADHANI KWANGAYA:
Naibu
Meya wa Jiji na Manispaa ya Ilala na Ubungo, Dar es Salaam wameendelea
kuwatumikia wananchi wao na kukitumikia Chama katika maeneo yao. Mhe.
Kumbilamoto ametoa Mashine ya Kuoshea magari kwa vijana wake wa
Vingunguti, Jezi seti tatu, na kufanya mkutano mkubwa wa hadhara
uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo kiongozi wa wabunge wa CUF
Bi. Riziki Shahali Ngw’ali, Mhe. Kuchauka na wadau wengine. Manaibu
Meya wamewatembelea waathirika wa Mafuriko katika maeneo mbalimbali ya
wilaya zao na Mhe Kwangaya amesimamia mradi wa uchimbaji wa visima vya
maji kwa wananchi wake wa wilaya ya Ubungo.
5. CHAMA
KIMETUMA SALAMU ZA RAMBIRAMBI NA KUTOA POLE KWA MSIBA WA WANAFUNZI 32
NA WALIMU ULIOTOKEA ARUSHA, NA KUWAPA POLE WANANCHI WALIOATHIRIKA NA
MAFURIKO KATIKA MAENEO MBALIMBALI NCHINI IKIWEMO TANGA, LUSHOTO, PEMBA
NA UNGUJA: Mhe
Saumu Sakala (MB) alikiwakilisha Chama katika msiba wa wanafunzi Jijini
Arusha. Aidha, Viongozi wa kambi ya CUF bungeni wameratibu safari za
wabunge kuwafikia wananchi katika majimbo yao kwa awamu ili kuwafariji
waathirika wa mafuriko hayo: waliokwenda Majimboni katika awamu hii ni
Mhe. Twahir Awesu Mohamed (Mkoani), Mhe. Khalifa Mohamed Issa (Mtambwe),
Hamad Salim Maalim (Kojani), Mhe. Dr, Suleiman Ali Yusuf (Mgogoni),
Mhe. Khatib Said Hajji (Konde), Mhe. Haji Khatib Kai (Micheweni), Mhe.
Mbarouk Salim Ali (Wete), Mhe. Abdallah Ally Mtolea (Temeke), na Mhe.
Yussuf Kaiza (Chakechake).
6. MWENENDO WA JESHI LA POILISI, UDHAIFU NA WOGA WA SERIKALI YA CCM YA AWAMU YA TANO KWA VYAMA KUFANYA SHUGHULI ZAKE ZA KISIASA:
Jeshi
la Polisi limekuwa likitumika vibaya kuhujumu shughuli za kisiasa
zilizoanishwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na
Sheria ya Vyama vya Siasa. Serikali ya CCM inayoongozwa na Rais
Magufuli imekuwa na UDHAIFU NA WOGA MKUBWA WA KUKOSOLEWA, KUHESHIMU
UTAWALA WA SHERIA NA KUFANYA VITENDO VYA KUKANDAMIZA DEMOKRASIA. Mbali
na kuzungumza mara kadhaa juu ya suala hili na viongozi wa Jeshi la
Polisi inaonekana pamoja na baadhi yao kuwa na nia njema na kuchoshwa na
mashinikizo yanayotokana na Viongozi wa Kisiasa wa Serikali ya CCM bado
vitendo hivyo vya kuihujumu CUF na viongozi wake vimekuwa vikiendelea
kwa kushirikiana na vibaraka wao ndani ya CUF. Ni Aibu kwa Serikali
inayojigamba kuwa imeshinda Uchaguzi kwa ridhaa ya wananchi kuogopa
vyama kufanya shughuli zake, kuogopa kukosolewa na kuzuia shughuli
halali za kisiasa za vyama. CUF inaendelea kulishughulikia suala hili na
kuhakikisha kuwa ufumbuzi wa kudumu unapatikana ili kuepusha machafuko
makubwa siku za usoni. Inashangaza kuona kuwa eti jeshi la Polisi
matahalani linapewa taarifa za kusudio la uvunjifu wa amani kwa barua na
watu wanaofahamika! Linaacha ‘kudeal’ na waliotoa taarifa hiyo
wanaokusudia kufanya vurugu, badala yake linajiandaa kutumia NGUVU KUBWA
na kuandaa vikosi vya majeshi kuzuia shughuli za Chama za kikao cha
ndani tu na wakati mwingine kiako hicho hakizidi watu 40. Tuna kila
sababu Vyama vya Upinzani nchini kufikiria njia mbadala za kukabiliana
na kukomesha hali hii.
7. USAFI OFISI KUU YA CHAMA BUGURUNI UPO PALEPALE:
Zoezi
la kufanya usafi katika ofisi kuu ya chama buguruni haliepukiki kutoka
na ofisi hiyo sasa kugeuzwa kichaka na kijiwe cha wahuni, kupanga na
kuratibu utekaji na kushambulia wananchi, wanachama na viongozi wa CUF,
uharibifu wa mali za chama, gari za Chama kutumika kwenda kuzikia
majambazi, kufanyika kwa vikao haramu, kukaribisha na kuwaficha wahalifu
mbalimbali na wengine wenye silaha za moto, Ofisi Kuu kugeuzwa Danguro
na makaazi ya wahalifu na waliokosa sehemu za kulala, kutumika kuanzisha
mradi wa mamalishe na kuonekana jungu la DONA likipikwa na kusababisha
uchafuzi wa mazingira, vyoo vimeharibiwa na hakuna usafi unaofanyika.
Kwa ufupi hakuna la maana linalofanyika kwa maslahi ya Chama cha CUF na
Taifa kwa ujumla. Lazima usafi ufanyike ili kuirejeshea heshima Ofisi ya
Chama. Mhe. Abdallah Mtolea (MB) kiongozi mratibu wa zoezi hilo
anawataka wana-CUF wote kuendelea na kufanya maandalizi ya kutosha
kutokana na makubaliano yetu na Viongozi husika kumalizika na hakuna
hatua zilizochukuliwa. Wakati wowote kuanzia sasa Mtajulishwa ni namna
ipi itumike kuondoa uchafu (Najisi) iliyojaa Ofisi Kuu, Buguruni.
HAKI SAWA KWA WOTE
------------------------------ ----------------
MBARALA MAHARAGANDE
NAIBU MKURUGENZI WA HABARI, UENEZI NA MAHUSIANO NA UMMA, CUF-TAIFA
MAWASILIANO: 0784 001 408/0715 062 577
Post a Comment