Na Daudi Manongi,MAELEZO,DODOMA.
Serikali kupitia Wizara ya
Viwanda,Biashara na Uwekezaji imeanzisha dawati la wepesi wa kufanya
biashara ambao lina jukumu la kuondoa ugumu wa kuanzisha na kuendesha
biashara nchini.
Hayo yamesemwa leo Bungeni na
Waziri wa Viwanda,Biashara na Uwekezaji Mhe.Charles Mwijage alipokuwa
akijibu swali la Mbunge wa Magomeni Mhe.Jamal Kassim Ali.
“Ujenzi wa Viwanda nchini
unategemea zaidi mazingira ya uwekezaji yaliyopo ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa ardhi yenye miundombinu wezeshi,sera mbalimbali,mifumo ya
kodi na mifumo ya upatikanaji wa vibali vinavyotakiwa kisheria ambayo
ni majukumu ya Serikali”Alisema Mhe.Mwijage.
Aidha Wizara ya Viwanda,Biashara
na Uwekezaji imeweka mikakati mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia
wafanyabiashara wa kitanzania ili kuwekeza kwenye viwanda hapa nchini.
Miongoni mwa Mikakati hiyo ni
Mafunzo yanayotolewa kwa watanzania wenye nia ya kuwekeza katika viwanda
juu ya kuibua mawazo ya kibiashara,kuanzisha ,kuendesha na kusimamia
biashara kupitia SIDO,kutoa ushauri wa kitaalamu wa jinsi ya kuchagua
teknolojia sahihi inayoendana na wazo la ujenzi wa kiwanda alilonalo
Mtanzania kupitia TIRDO,TEMDO na CAMARTEC na namna ya kupata ama kukuza
mtaji wa ujenzi wa viwanda kupitia NEDF,SIDO na TIB.
Pamoja na hayo Wizara imeandaa
mwongozo kwa Mikoa,Wilaya,Kata na Vijiji kutenga maeneo ,kusimamia
sheria,kanuni,taratibu na kutoa maelekezo kwa wawekezaji.
“Watanzania wnaaotaka ama walio na
mitaji mikubwa wanaweza kuwekeza kupitia maeneo ya EPZA ambayo
yametengwa mahsusi kwa ajili ya uzalishaji wa bidhaa zinazouzwa nje ya
nchi,Pia wanaweza kuwasiliana na TIC kupata vivutio mbalimbali
vilivyowekwa na Serikali kwa ajili ya uwekezaji,Alisisitiza Mhe.Mwijage.
Post a Comment