Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali imetoa asilimia miamoja
ya fedha za bajeti ya dawa kwa mwaka 2016/2017 kwa ajili ya manunuzi
ya dawa ikiwa ni moja ya mikakati ya kuboresha sekta ya afya nchini.
Akizungumza katika mahojiano ya
kipindi cha TUNATEKELEZA kinachoratibiwa na Idara ya Habari – MAELEZO na
kurushwa na kituo cha televisheni cha TBC, Mkurugenzi Mkuu wa Bohari
Kuu ya Dawa Laurean Bwanakunu alisema kuwa serikali inawahakikishia
wananchi kuwa katika mwaka wa fedha 2016/2017 imetenga fedha za kutosha
ili kuhakikisha kuwa dawa zinapatikana katika vituo vya kutolea huduma
za afya.
“Ikiwa ni asilimia 81 ya
upatikanaji wa dawa pamoja na vifaa tiba katika maeneo ya mjini na
vijijini, ambapo Bohari Kuu ya Dawa inahudumia vituo 5642 nchi kote”
alisema Bwanakunu.
Pia, Bwanakunu alibainisha kuwa
hivi sasa kumekuwepo na upatikanaji wa dawa muhimu 110 kati ya 135
katika vituo mbalimbali vinavyotoa huduma za huduma za afya.
Katika kuboresha huduma za
usambazaji wa dawa nchini , Bohari Kuu ya Dawa imefanikiwa kufungua
maduka ya dawa 7 katika mikoa ya Dar es salaam, Arusha, Geita, Mbeya na
Lindi, ambapo imeanza kusafirisha dawa kwa kutumia ndege na treni ili
kufikisha dawa kwa wakati katika vituo mbalimbali vya afya nchini.
Aidha, Mikoa na Halmashauri
zimetakiwa kuwasilisha maombi yao ya dawa kwa wakati ili kutatua
changamoto ya upungufu wa dawa katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Post a Comment