Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
Pamoja
na malalamiko na manung’uniko ya hali ngumu ya maisha kwa watanzania
wengi, Tanzania ndio yenye kiwango cha chini cha mfumuko wa bei wa
wastani wa asilimia 6.1 kwa mwezi Mei 2017 kwa nchi za Afrika Mashariki.
Hayo
yamebainishwa leo bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Fedha na Mipango
Dkt. Philip Mpango akiwasilisha Taarifa ya Hali ya Uchumi wa Taifa kwa
mwaka 2016 na Mpango wa Maendeleo kwa mwaka 2017/18.
Mhe.
Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei katika nchi za Afrika Mashariki kwa
mwaka 2016 uliendelea kuwa wa kiwango cha tarakimu moja, ambapo Rwanda
ilikuwa na asilimia 7.1, Uganda asilimia 5.4, Tanzania asilimia 5.2,
Kenya asilimia 6.3 na Burundi asilimia 5.6.
Alisema
kufikia mwezi Aprili 2017, mfumuko wa bei kwa nchi hizi ulipanda,
ambapo kwa Burundi ulifikia asilimia 21.10, Rwanda asilimia 13.0; Kenya
asilimia 10.28; Uganda asilimia 6.4 na Tanzania asilimia 6.4.
“Hata hivyo, kwa upande wa Tanzania mfumuko wa bei umeendelea kushuka mpaka asilimia 6.1 kwa mwei Mei 2017” amesema Dkt. Mpango
Mhe.
Dkt Mpango amesema kwa miaka minne mfululizo, wastani wa mfumuko wa
bei kwa Tanzania umeendelea kupungua, ukibaki katika kiwango cha
tarakimu moja.
Amesema
kwa mwaka 2016, mfumuko wa bei ulifikia wastani wa asilimia 5.2
ikilinganishwa na asilimia 5.6 mwaka 2015. Kupungua kwa wastani wa
mfumuko wa bei nchini kulichangiwa kwa kiasi kikubwa na: mwenendo wa
kushuka kwa bei za mafuta ya petroli katika soko la dunia na nchini;
kuimarika kwa upatikanaji wa vyakula nchini na hivyo kuimarisha wastani
wa bei; na kuwepo kwa sera madhubuti za usimamizi wa bajeti na fedha.
Mhe.
Dkt. Mpango amesema mfumuko wa bei uliongezeka kidogo, ambapo ulifikia
asilimia 6.4 mwezi Aprili 2017 lakini ukiwa ndani ya maoteo ya wastani
wa tarakimu moja (asilimia 5 – 8) kwa mwaka 2017.
Hali
ya kuongezeka kwa mfumuko wa bei nchini ilichangiwa na hofu iliyotokana
na kuchelewa kwa msimu wa mvua katika maeneo mengi nchini na hivyo
kuwepo kwa taharuki ya kutokea upungufu wa chakula. Hata hivyo, maeneo
mengi yamepata mvua ya kutosha na hivyo bei ya chakula nchini
inatarajiwa kupungua.
Mhe.
Dkt. Mpango amesema kasi ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya ya Afrika
Mashariki ilishuka kutoka wastani wa asilimia 6.5 mwaka 2015 hadi
asilimia 5.3 mwaka 2016 ijapokuwa Jumuiya hii iliendelea kuongoza kwa
ukuaji miongoni mwa Jumuiya mbalimbali za Afrika.
Amesema
kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii ilichangiwa na sababu
mbalimbali ikiwemo kushuka kwa bei za bidhaa na kudorora kwa uchumi wa
dunia. Maoteo ya mwenendo wa uchumi katika ukanda huu yanaonesha utakua
kwa wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2017 na asilimia 6.0 mwaka 2018.
“Matarajio
haya yanazingatia hatua zinazochukuliwa na nchi za ukanda huu katika
kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara kama vile kuwa
na maeneo tengefu ya ujenzi wa viwanda (industrial parks), hususan, vya
nguo, bidhaa za ngozi, kilimo, madawa na vifaa tiba” ameongeza Dkt. Dkt.
Mpango
Amesema
kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kasi ya
ukuaji wa uchumi ilishuka kutoka wastani wa asilimia 1.9 mwaka 2015 hadi
asilimia 1.1 mwaka 2016.
Mhe.
Dkt. Mpango amesema kasi ndogo ya ukuaji wa uchumi katika Jumuiya hii
ilichangiwa na uhaba wa nishati ya umeme pamoja na ukame uliochangiwa na
mabadiliko ya hali ya hewa ya La Nina.
Amesema
licha ya kasi ndogo ya ukuaji, Jumuiya hii iliendelea kuwa ya tatu kwa
ukuaji miongoni mwa Jumuiya za barani Afrika na unatarajiwa kukua kwa
wastani wa asilimia 1.4 mwaka 2017.
Waziri
wa Fedha amesema mfumuko wa bei ulifikia asilimia 10.5 mwaka 2016
ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 2015, ukichangiwa na ukame na
kuyumba kwa utekelezaji wa sera za mapato na matumizi kwa baadhi ya nchi
wanachama.
Ameeleza
kuwa matarajio katika nchi hizo ni kuwa kwa mwaka 2017 mfumuko wa bei
utapungua hadi kufikia asilimia 8.7 kutokana na kushuka kwa gharama za
bidhaa, kuimarika kwa upatikanaji wa nishati ya umeme, na uthabiti wa
bei ya mafuta; na kuimarika kwa hali ya hewa.
Post a Comment