Na Immaculate Makilika.
Soko
la pamoja la Afrika Mashariki linalenga kupanua na kuimarisha
ushirikiano wa kiuchumi na kijamii miongoni mwa nchi wananchama kwa
maslahi yao. Hii inatoa fursa kwa raia wote na hasa Watanzania ambao
wanaonekana hawafahamu ama hawatumii fursa hizo kama raia wengine wa
nchi wanachama.
Ryunosuke
Satoro, mwandishi maarufu wa nchini Japan aliyezaliwa mwaka 1892
aliwahi kusema “Individually, we are one drop. Together, we are an
ocean” , msemo huu una maana kwamba nguvu ya mtu mmoja ni kama tone la
maji na nguvu ya watu wengi ni mithili ya bahari, kwa hivyo mafanikio
madhubuti hupatikana ikiwa watu watashirikiana ama kufanya kazi kwa
pamoja.
Msemo
huu unajibu dhima mahsusi ya chimbuko la kuanzishwa kwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki. Kwa mujibu wa ibara ndogo ya za 76(1) na 104 (2) za
Mkataba wa kuanzisha Jumuiya hii, ambayo maeneo ya msingi yaliyohusishwa
katika soko hilo la pamoja ni Soko huru la bidhaa ndani ya Jumuiya,
Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kusafiri katika nchi yoyote ndani ya
Jumuiya na Uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya kazi katika nchi
yoyote ndani ya Jumuiya hiyo.
Kwa
uhalisia Watanzania wanaonekana ni raia wasiochangamkia fursa hizo kwa
karibu ukilinganisha na raia wa nchi zingine, hii inaweza kusababishwa
na kutofahamu kabisa fursa zilizoko au kuwa na uelewa mdogo. Katika
makala hii mwandishi analenga anatoa elimu kwa Watanzania kuhusu
fursa hizo, kwa kuweka kuelezea soko lenyewe, faida zake na maeneo
ambayo Watanzania wanaweza kunufaika nayo.
Soko
huru la bidhaa linasimamiwa na itifaki ya umoja wa forodha na sheria ya
Afrika Mashariki ya Usimamizi wa shughuli za forodha ya mwaka 2004,
ambapo kuanzia Januari mosi mwaka 2010, bidhaa zote zinazozalishwa ndani
ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kukidhi vigezo vya utambuzi wa uasili
wake zinaweza kusafirishwa kutoka nchi moja hadi nyingine bila kutozwa
ushuru wa forodha.
Ibara
ya 7 ya itifaki ya soko la Afrika Mashariki inaruhusu raia yoyote wa
nchi wanachama kusafiri katika nchi yoyote miongoni mwa nchi za Jumuiya
na kupata ulinzi na usalama bila kubaguliwa kwa misingi ya utaifa ikiwa
ni pamoja na kupata huduma za matibabu na masomo.
Aidha,
raia anayetaka kunufaika na uhuru huo wa kusafiri anatakiwa kuwa na
kibali maalumu kutoka vyombo husika katika kila nchi. Pia, soko hilo la
pamoja linatoa uhuru wa raia wa Afrika Mashariki kufanya kazi katika
nchi yoyote ndani ya Jumuiya hiyo. Lengo la uhuru huo ni kutoa fursa za
ajira kwa raia wa nchi wanachama.
Raia
wa nchi za Jumuiya wanatakiwa kuzingatia mfumo uliokubalika kwa kuunda
soko la pamoja, ambapo kila nchi imeainisha kada zilizohusishwa na
ufunguaji wa soko la ajira. Kwa msingi huo wanajumuiya wanaruhusiwa
kutafuta ajira ndani ya maeneo hayo.
Kupitia
makubaliano hayo, Watanzania wana nafasi ya kwenda kufanya biashara
katika nchi nyingine za Jumuiya bila kuzuiwa, na hivyo kutumia fursa
hiyo kusambaza biashara zao na kupata nafasi ya kubadilishana mawazo na
wafanyabishara wenzao ndani ya Jumuiya.
Katika
kuunga mkono ushirikiano ndani ya Jumuiya, aliyekuwa Mwenyekiti wa
wabunge wa Tanzania katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA), Makongoro
Nyerere, alitoa wito kwa Watanzania kuchangamkia nafasi zilizopo za
kufanya biashara katika nchi za Afrika Mashariki, na kwamba wananchi
wajitahidi kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu soko hilo.
Watanzania
wanaweza kuchangamkia fursa hizo katika sekta ya elimu, kwa nafasi ya
walimu kuanzia ngazi ya shule ya msingi zinazofundisha kingereza hadi
Vyuo vikuu, sekta ya kilimo, kwa nafasi ya walimu wa vyuo vya kilimo,
maafisa ugani na ufundi stadi kwa ngazi ya shahada ya pili, wauguzi,
wakunga na wahudumu wengine wa sekta ya Afya.
Aidha, fursa nyingine za ajira ni uhandisi wa madini, majengo, waongoza ndege na upimaji ramani.
Ili
kutilia mkazo suala hilo, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki kupitia Msemaji wake Mindi Kasiga amesema
wafanyabiashara wa Tanzania wanatakiwa kutumia fursa za biashara
zinazopatikana katika soko la nchi wanachama wa Jumuiya kwa kuuza
bidhaa zao ndani ya Jumuiya hiyo.
“Wafanyabiashara
wanatakiwa kuchangamkia fursa ya biashara katika soko la pamoja kwa
kuwa ni haki yao na ni utekelezaji wa malengo ya mkataba wa uanzishwaji
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kifungu cha tano ambacho kilianzisha
itifaki ya umoja wa forodha” anasisitiza Mindi.
Aidha,
wizara inawataka wafanyabiashara kutoa taarifa endapo watakumbana na
vikwazo visivyo vya kiforodha kupitia mfumo wa ujumbe mfupi kwa kuandika
neno ‘NTB’ kwenda namba 15539, ambapo imeandaa utaratibu wa kutatua
changamoto hizo.
Ni
matarajio ya Jumuiya kuwa fursa hizo zinaweza kupunguza tatizo la ajira
kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo Watanzania wamekuwa wakikabiliana nalo
kwa muda, kwa vile ni dhahiri kuwa Serikali haina uwezo kutoa ajira kwa
kila mwenye uhitaji kwa hivyo hii ni fursa adhimu kwa watanzania kutumia
ujuzi, taaluma na mitaji ili kulikabili soko hili la pamoja.
Ushiriki
wa Watanzania katika soko hili utawaongezea kipato mtu mmoja mmoja,
itatoa fursa ya kujifunza kutoka kwa raia wananchama wa jumuiya hiyo
ikiwa ni pamoja na kujiongezea ujuzi katika nyanja mbalimbali, sambamba
na kufikia malengo ya nchi ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumu wa
kati ifikapo mwaka 2025.
Post a Comment