WANAHABARI WA ISRAEL WATEMBELEA HIFADHI YA TAIFA YA GOMBE, WAAHIDI KUTANGAZA VIVUTIO VYA TANZANIA NCHINI HUMO
Kundi la waandishi kumi wa habari kutoka nchini Israel wakiwa katika hifadhi ya Taifa ya Gombe hivi karibuni kwa ajili ya kurekodi vivutio mbalimbali vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo kwa ajili ya kuvitangaza nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Hifadhi za Taifa (TANAPA). Kwa sasa soko la utalii la mashariki ya kati limeanza kufunguka kwa kasi ambapo hivi karibuni Waziri Mkuu Mstaafu wa Israel Ehud Barak ametembelea hifadhi za Ngorongoro na Serengeti.
HAMZA TEMBA - WMU
Kundi la wanahabari kumi akiwemo muigizaji mmoja na maofisa wa kampuni ya utalii ya Safari kutoka nchini Israel limetembelea hifadhi ya Taifa ya Gombe iliyopo mkoani Kigoma na kufurahia vivutio lukuki vya utalii vinavyopatikana katika hifadhi hiyo na kuahidi kuvitangaza watakaporudi nchini kwao ikiwa ni mkakati wa Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia TANAPA na Bodi ya Utalii kutangaza vivutio hivyo nchini humo.
Akizungumza hivi karibuni mara baada ya kukamilika kwa ziara hiyo ya siku mbili, Kiongozi wa kundi hilo, Ronit Hershkovitz alisema ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa ambapo wamefurahia kuona vivutio vya kipekee katika hifadhi hiyo na kuahidi kuwa mabalozi wazuri wa vivutio hivyo nchini Israel.
Timu maalum ya wanahabari kutoka nchini Israel ikiwa na wajumbe kumi ilipowasili katika uwanja wa ndege wa Kigoma tayari kwa ajili ya ziara ya kitalii ya siku mbili katika hifadhi ya Taifa ya Gombe. Ziaza hiyo iliandaliwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kwa kushirikiana na Shirika ya Hifadhi za Taifa Tanzani (TANAPA) kwa ajili ya kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Israel ikiwa ni mkakati maamlum wa kukamata soko la Mashariki ya Kati. Kutoka kulia wanaongoza msafara huo ni Meneja Mawasiliano TANAPA, Paschal Shelutete na Meneja Mahusiano wa TTB, Geofrey Tengeneza.
“Ni furaha kubwa kuwa hapa Gombe, tumeona makundi ya Sokwe na fukwe nzuri za Ziwa Tanganyika, tuko hapa kwa ajili ya kwenda kueleza kivutio hiki na vivutio vingine vya Tanzania nchini Israel, Waisrael wanaipenda Tanzania na wanapenda kutembelea Tanzania, tumeona ongezeko kubwa la watalii katika miaka ya hivi karibuni kutoka Israel baada ya kazi ngumu ya muda mrefu, sasa tuna furaha kuona watalii wengi wanaongezeka na tungependa kuona pia Watanzania wengi wakitembelea Israel,” Alisema Ronit.
Aliongeza kuwa, “Tunaenda kueleza taarifa hizi kwenye mitandao ya kijamii, magazeti, televisheni na popote tutakapoweza, lakini kubwa zaidi ni kuwaeleza marafiki zetu ana kwa ana uzuri wa Tanzania kwasababu tunaipenda Tanzania, nakupenda sana”.
Wanahabari kutoka Israel wakipanda kwenye boti kwa ajili kunza safari kuelekea hifadhi ya Taifa ya Gombe. Msafara huo ulikuwa na wanahabari kutoka vyombo maarufu nchini humo ikiwemo kituo cha Televisheni cha Channel 2, Jarida la Atmosphere, Jarida la National Geographic, Jaria la wiki la Yediot Acharanot -7 Yamim na waandishi wawili wa mitandao ya kijamii. Wengine ni maofisa wawili wa kampuni ya Utalii ya Safari ya nchini humo.
Walfson Noa, ambaye ni Mwandishi wa Mitandao ya Kijamii na Meneja Masoko wa Kampuni ya Utalii ya Safari ya Israel alisema, “Tulifanya matembezi kuwaona Sokwe wanaovutia sana huku wakiishi katika mazingira yao ya asili, hili ziwa ni la maajabu sana (Ziwa Tanganyika), hata nyani nao walikuwa wakijaribu kuingia kwenye mahema yetu ni jambo la kuvutia, katika mtizamo wa kimasoko hili ni eneo ambalo nitawashauri wateja wangu watembelee, ni kitu ambacho watu wanatakiwa kukifahamu, kugundua siri ya uzuri wa hifadhi ya Taifa ya Gombe”
Post a Comment