HOTUBA YA MHESHIMIWA UMMY MWALIMU
(MB), WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KATIKA
UFUNGUZI WA MKUTANO WA KWANZA WA KUPITIA UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA
UBORESHAJI WA KASI YA UIBUAJI WA WAGONJWA WA KIFUA KIKUU NCHINI, KATIKA
UKUMBI WA KILIMANI LANDMARK, DODOMA, JULAI 4, 2017
- Katibu Mkuu wamjw,
- Naibu Katibu Mkuu OR-TAMISEMI ,
- Mganga Mkuu Kiongozi,
- Wajumbe kutoka Global Fund,
- Wakurugenzi na Wawakilishi wa USAID, CDC, EGPAF, AGPAHI, Save the Children, FHI, MDH, AMREF, KNCV, Delloite, Baylor, Water Reeds na wengine,
- Wakurugenzi kutoka TAMISEMI na WAMJW,
- Mameneja Mipango ya NTLP, RCH na NACP,
- Waganga Wakuu wa Mikoa na Waganga Wakuu wa Wilaya,
- Waratibu wa Mikoa na Wilaya wa TB na Ukoma na TBHIV,
- Watoa huduma kutoka Vituo vya Afya katika Halmashauri,
- Waandishi wa Habari,
- Waalikwa wote,
- Mabibi na Mabwana.
Awali ya yote nitumie fursa
hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia afya njema
na kutuwezesha kukutana hapa. Pili, niwashukuru waandaaji kwa kunialika
katika mkutano huu muhimu; mkutano wa kwanza wa kitaifa wa kufanya
mapitio ya utekelezaji wa mkakati wa uboreshaji wa kasi ya uibuaji wa
wagonjwa wa kifua kikuu. Hii ni hatua muhimu kujiangalia na kuona njia
tunayopitia katika juhudi za kuhakikisha tunawafikia kila mwenye uhitaji
wa huduma za matibabu ya kifua kikuu. Vile vile, nitumie fursa hii
kuwakaribisha wajumbe wote na nawapongeza kwa kuchukua muda wenu kuja
kuhudhuria kikao kazi hiki muhimu. Natambua pia ya kuwa kuna wajumbe
wengine wamesafiri umbali mkubwa na wengine wametoka nje ya nchi;
“napenda kusema wote karibuni sana hapa Dodoma, makao makuu ya nchi
yetu”.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Utoaji wa huduma za afya
usiozingatia ubora huathiri kila mtu, si tu wateja na wagonjwa wetu,
hata sisi watoa huduma. Huduma zikiwa mbovu zinawafanya hata
wanaozihitaji kukata tamaa na kutojitokeza vituoni. Malengo Endelevu ya
Maendeleo na mkakati wa Dunia wa kutokomeza kifua kikuu (End TB
Strategy) yametilia mkazo utoaji wa huduma za afya zenye ubora wa hali
ya juu na kwamba si budi juhudi za makusudi kufanyika ili kila mhitaji
kufikiwa. Masuala ya ubora wa huduma za afya yamepewa kipaumbele katika
mkakati mpya uliotolewa na Shirika la Afya Duniani wa kutokomeza kifua
kikuu ifikapo mwaka 2035. Wakati huo huo, kikao cha Baraza la Shirika la
Afya Duniani kilochoketi mwezi uliopita kimeziagiza nchi wanachama na
Shirika la Afya Duniani (WHO) kutilia mkazo wa kipekee mipango yakinifu
ya ubora katika utoaji huduma zote za afya. Kikao hicho, kimewataka
wahisani na mashirika yenye uwezo kuzisaidia nchi zenye uhitaji ili
kuzijengea ujuzi wa kuboresha misingi ya huduma bora za afya.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Changamoto kubwa tuliyonayo hapa
kwetu Tanzania, ni kutoweza kuifikia sehemu kubwa ya wagonjwa wa kifua
kikuu. Kiasi cha wagonjwa zaidi ya 100,000 wa kifua kikuu hatuwafikii
kila mwaka. Licha ya kuwa na mazingira yaliyosawa na maeneo mengine
mfano katika Mikoa ya Rukwa, Katavi, Simiyu, Shinyanga, Kigoma, Kagera,
Dodoma, Iringa, Mara na Singida inagundua wagonjwa wachache sana
ikilinganishwa na Mikoa ya Mbeya, Lindi, Mtwara na Tanga. Tafiti nyingi
zimeonyesha kwamba, tunahitaji mbinu mpya za kuboresha huduma
tunazozitoa ili kuhakikisha kila mgonjwa na mteja anayekuja katika vituo
vyetu vya huduma anapata fursa ya kuchunguzwa kikamilifu ili kubaini
kama anaugua kifua kikuu au la.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Mkakati wa uboreshaji kasi ya
uibuaji wagonjwa wa kifua kikuu ni mkakati uliojaa mbinu za kiuendeshaji
ili kuvipa uwezo vituo vyetu vya huduma kufanya uchunguzi wa kina kwa
kila mteja anayepata huduma vituoni na kuwapata wote wenye kuugua kifua
kikuu na kuwaanzishia matibabu. Mathalan, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Dodoma katika miezi sita baada ya kuanza kutekeleza mkakati huu
wameongeza wastani wa kuibua wagonjwa wa kifua kikuu kutoka 28 hadi 54
kwa mwezi. Tunahitaji kubadili mtazamo wetu na utendaji kazi wetu hasa
suala zima la kuhakikisha tunafanya upekuzi na uchunguzi wa wagonjwa
vituoni, tusingoje mgonjwa atufuate na kutueleza dalili za kifua kikuu
akiwa kituoni, hivyo ni vyema juhudi zetu zianzie kuwatambua wagonjwa
hawa katika jamii.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Ili kuhakikisha tunaweka misingi
mizuri ya utekelezaji wa mkakati huu, Wizara ikishirikiana na Global
Fund, imetengeneza kitita kiongozi ili kutoa mwongozo kwa watoa huduma
katika kila kitengo na kliniki ndani ya vituo vya huduma jinsi ya
kufanya hatua kwa hatua kubaini kifua kikuu kwa kila mwenye kugua bila
kukosa. Mkakati huu muhimu unatoa fursa kwa kila kitengo kujitathmini
ili kuweka misingi timilifu ya uchunguzi wa kifua kikuu kwa wateja wote
wanaohudhuria matibabu katika eneo lao. Kitita hiki kinaviwezesha vituo
vyetu vya huduma kumfikia kila mmoja mwenye uhitaji wa uchunguzi wa
kifua kikuu, kutoa huduma zinazozingatia usawa, usalama wa mgonjwa au
mteja na huduma zinazokidhi viwango vya Kimataifa.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Tunao wajibu wa kuhakikisha
mkakati huu unatekelezwa kwa ufanisi uliokusudiwa, ili tufikie lengo
hilo, Wizara kwa mara ya kwanza imeanzisha rejesta mpya ya wanaohisiwa
kuwa na kifua kikuu itakayowekwa katika kila ngazi ya utoaji wa huduma
za Afya hapa nchini. Tayari rejesta hizi zimesambazwa na kuanza kutumika
katika mikoa 16 iliyoanza kutekeleza zoezi hili. Kesho kutwa, wote hapa
tutashuhudia kuzinduliwa kwa mkakati huu maalumu wa uboreshaji huduma
za uibuaji wagonjwa wa kifua kikuu katika Halmashauri. Zana hizi
zitatoa mwanga na kuangaza njia bora za kuchunguza kifua kikuu na
kubaini wote wenye kuugua katika jamii yetu mijini na vijijini.
Mafanikio endelevu ya mkakati huu, yanategemea jinsi tutakavyojipanga
kuanzia ngazi ya zahanati hadi wasimamizi ngazi ya kitaifa katika Wizara
ya Afya na TAMISEMI. Mbinu zinazoelekezwa ni za kawaida, nyepesi na
zinaeleweka vizuri na utekelezaji wake utaleta matokeo chanya na unaweza
kufikiwa na kila mtoa huduma. Kazi zilizoainishwa katika kutekeleza
mkakati huu zinatoa chagizo kwa watoa huduma vituoni na wasimamizi
kuwajibika kikamilifu, kila mmoja katika nafasi yake na kujenga timu
imara katika kila eneo la kazi.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Nimetaarifiwa kuwa, utekelezaji wa
mkakati huu ulianza mnamo Julai, 2016, ambapo ni mwaka mmoja sasa tokea
vituo vya mwanzo katika Mikoa ya Mbeya na Dodoma ianze kuweka msukumo
mpya. Kuanzia hapo, Mikoa 16, wilaya 48 na vituo 187 nchini kote
vimeweza kuanza utekelezaji. Katika mkutano huu wa kwanza wa kufanya
mapitio na tathmini ya utekelezaji wa mkakati huu, ninafarijika kuwa
umehudhuriwa na wajumbe wa RHMT na CHMT na watumishi kutoka vituo vya
huduma katika Mikoa hiyo yote 16 ambao wote ni walengwa wakuu katika
kufanikisha jukumu hili.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Napenda kubainisha changamoto
mbili kuu tunazo hitaji kukabiliana nazo, Moja, kuanzisha mfumo imara wa
ufuatiliaji na usimamizi elekezi, Pili, ni kuhakikisha tunatoa
usimamizi imara na wenye tija katika kuimarisha ufanyaji kazi kama timu
ya ushindi na kuvifanya vituo vyetu kutoa huduma kwa wagonjwa wa kifua
kikuu zilizo za bora na endelevu. Kufikia hatua hizi yatubidi kuimarisha
timu za uboreshaji huduma vituoni (Quality Improvement teams – QIT) na
kuzipa uwezo zaidi wa kusimamia viwango vya ubora wa huduma za afya
katika maeneo yao ya kazi vituoni, hospitali na vituo vya ngazi za chini
pia.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Napenda kuwaaminisha ya kuwa,
tukiweza kuwabaini wale wanaofanya vizuri zaidi katika vituo vilivyo
katika Halmashauri zetu na tukawatumia kueneza utendaji wao mzuri katika
maeneo mengine inaweza kuleta matokeo chanya kwa haraka na kupata
mafanikio endelevu. Watendaji bingwa hawa, watatusaidia kurahisisha
hatua za ugatuzi na kupanua huduma hizi katika nchi nzima. Ili mpango
huu ulete mafanikio tunayoyatarajia, inabidi timu za uendeshaji za Mikoa
na Halmashauri kuwapa kila msaada ili wafanye vizuri zaidi na
kuimarisha ubora wa mfumo mzima wa afya katika maeneo yetu.
Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana,
Mkakati huu na utekelezaji wa kazi
nyingine za kuimarisha mfumo wetu wa huduma bora za afya hatuwezi
kuvifanya peke yetu; yatubidi kuzitelekeleza katika ushirika wa pamoja
kati ya Serikali na wadau wetu. Ni napenda kutumia fursa hii,
kuwashukuru wadu wetu wa maendeleo kwa ushirikiano na misaada
mnayoendelea kutupatia. Wote kwa pamoja tunawashukuru sana.
Hitimisho:
Kwa mara nyingine tena nitumie
fursa hii kuwashukuru wadau wa maendeleo kwa kutusaidia kuimarisha
miundo mbinu ya Afya, mifumo ya uendeshaji huduma za afya na udhibiti wa
magonjwa mbali mbali yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria. Ni imani
yangu pia ya kuwa ushikaino huu utazidi kuimarika na kusonga mbele ili
tuweze kuboresha utoaji wa huduma za Afya. Ni imani yangu vile vile
kwamba kongamano hili ni fursa ya kipekee kubadilishana uzoefu wa namna
ya kutenda kazi kwa ufanisi wa hali ya juu katika kuibua mbinu bunifu
mbali mbali ili kuboresha huduma katika mikoa na Halmashauri zetu.
Baada ya kusema haya machache, sasa napenda kutamka rasmi kuwa, mkutano huu umefunguliwa.
Asanteni kwa kunisikiliza.
Post a Comment