Taasisi ya Kimataifa ya Kijamii ya
Uhifadhi wa Wanyamapori (WCS) imetoa msaada wa zaidi ya shilingi milioni
940 ambazo zimetumika kujenga ofisi, kununua vitendea kazi yakiwemo
magari na kughamaramia mafunzo kwa askari wa wanyamapori wa mapori ya
akiba ya lukwati- piti ili kukabiliana na ujangili na uwindaji haramu
ambao umesababisha vifo vya tembo wapatao 23 tangu mwaka 2013 mpaka
sasa.
Meneja wa mapori hayo ya akiba ya
lukwati/ piti Alphonce Ambroce Mung’ong’o amesema mapori hayo mawili
yenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 6,119 yaliyoko Lupa
Tingatinga mkoani Songwe yanatumika kwa uwindaji wa kitalii wa
wanyamapori ambayo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita
yameiingizia serikali mapato ya zaidi ya dola za kimarekani milioni 1.3
sawa na zaidi ya shilingi bilioni mbili na milioni mia nane na amewaonya
watu wanaojihusisha na ujangili kuwa sasa watafute kazi nyingine:
Akiongea katika hafla ya kukabidhi
miradi hiyo ikiwemo jengo la kisasa, magari na vifaa vya doria kwa
serikali ya Tanzania, Mkurugenzi wa WCS, Aaron Nicholaus amesema WCS
inajivunia kushirikiana na serikali ya Tanzania katika kuimarisha
uhifadhi.
Pia amezungumzia umuhimu wa mapito ya
wanyamapori ambayo yameathiriwa na shughuli za binadamu licha ya umuhimu
wake kwa uhifadhi ambapo katibu mkuu wizara ya maliasili na utalii meja
jenerali gaudance milanzi amesema msimamo wa serikali katika uhifadhi
uko wazi kwani maliasili hizo zina umuhimu kwa maendeleo ya taifa.
Kaimu Mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya
wanyamapori tanzania tawa, martin loibooki amesema tawa inatambua wajibu
wake na malengo ya kuanzishwa kwa mamlaka hiyo ya kusaidia kuchochea
maendeleo ya jamii na kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya wanyamapori
na ameishukuru wcs kwa kuwa mfadhili wa kwanza kufadhili shughuli za
uhifadhi katika mapori ya lukwati- piti
Post a Comment