TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 26.07.2017.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya
limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo
mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana
na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na
uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na
kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Mafanikio yaliyopatikana kutokana na misako ni kama ifuatavyo:-
KUPATIKANA NA RISASI ZA SHORT GUN.
Mnamo tarehe 25.07.2017 majira ya
saa 21:05 Usiku Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko
katika Pori lililopo Kitongoji cha Nzombo kandokando ya Mto Songwe, Kata
ya Bonde la Usongwe, Tarafa ya Usongwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini na
kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la NELSON TUYANJE @
MWAIGOMBE [47] Mkazi wa Kijiji cha Mwampalala kilichopo Kata ya Iwindi
akiwa na risasi sita (06) za Short Gun aina ya Melior Super GT.
Awali Jeshi la Polisi lilipata
taarifa toka kwa raia wema kuwa kuna watu wawili wameonekana katika
pori hilo wakiwa na silaha ndani ya mfuko wa salfeti. Aidha silaha hiyo
haijapatikana baada ya mtu mmoja ambaye bado anatafutwa kudaiwa kuwa
ndiye mmiliki halali wa silaha hiyo kutoonekana mara baada ya mwenzie
kukamatwa na yeye kufanikiwa kutokomea porini. Upelelezi unaendelea
pamoja na msako mkali wa kumtafuta mtuhumiwa aliyekimbia.
Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa
Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na
wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha
Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na tukio 01 la
Ajali ya Moto lililosababisha kifo cha mtu mmoja kama ifuatavyo:-
AJALI YA MOTO NA KUSABABISHA KIFO.
Mnamo tarehe 25.07.2017 majira ya
saa 23:45 usiku huko Mnarani Forest Mpya, Kata ya Forest, Tarafa ya
Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la
MAGRETH KAMBONJA [46] Mwalimu wa Shule ya Msingi Mkombozi iliyopo
Mbalizi, aliuguliwa na nyumba yake yenye vyumba vinne na kuteketeza
mali zote zilizokuwa katika nyumba hiyo na kusababisha kifo cha mwenye
nyumba hiyo MAGRETH KAMBONJA.
Inadaiwa kuwa chanzo cha kifo
chake ni kutokana na kuvuta moshi mwingi hali iliyopelekea kufariki
dunia wakati alipokuwa akipelekwa Hospitali kwa matibabu. Chanzo cha
moto huo inasemekana ni hitilafu ya umeme iliyosababishwa na jokofu
[fridge] iliyokuwa ikigandisha barafu. Moto huo umezimwa kwa
ushirikiano wa wananchi, Jeshi la Polisi na Kikosi cha zima moto.
Upelelezi unaendelea.
KUMWAGIWA KIMIMINIKA KINACHODHANIWA KUWA TINDIKALI
Mnamo tarehe 19.07.2017 majira ya
saa 21:30 usiku huko eneo la Manga lililopo Tarafa ya Sisimba, Jiji na
Mkoa wa Mbeya, mama mmoja aliyefahamika kwa jina la VUMILIA SHANGEMA
[31] Mfanyabiashara na Mkazi wa Manga akiwa amefuatana na watoto wake
wawili 1. LOVENESS JOHN [11] Mwanafunzi wa Darasa la Sita katika Shule
ya Msingi Sinde na 2. NANCY PETER [05] walijeruhiwa kwa kumwagiwa usoni,
kifuani na mkononi kimiminika kinachodhaniwa kuwa ni tindikali.
Inadaiwa kuwa siku ya tukio
mhanga ambaye ni VUMILIA SHANGEMA akiwa amefuatana na watoto wake wawili
wakitokea dukani kununua bidhaa kwa ajili ya matumizi ya nyumbani
wakiwa njiani alitokea mama mmoja ambaye aliweza kufahamika kwa jina la
EMMY KYANDO [40] Mkazi wa Sae Jijini Mbeya ambaye inadaiwa kuwa ni mke
mwenza na mhanga kutokana na mhanga kudai alizaa mtoto mmoja aitwaye
LOVENESS JOHN na mume wake.
Mara baada ya mama huyo
kujitokeza maeneo hayo aliwamwagia kimiminika hicho sehemu za usoni,
kifuani na mikononi. Wahanga walipata msaada toka kwa wasamaria wema wa
kupelekwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu. Aidha mhanga VUMILIA
SHANGEMA ameumia vibaya usoni na kwenye macho hali inayosababisha
kutoona. Majeruhi mwingine LOVENESS JOHN alijeruhiwa usoni lakini hali
yake sio mbaya sana, NANCY PETER alitibiwa na kuruhusiwa.
Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio
hilo ni wivu wa kimapenzi. Juhudi za kumtafuta mtuhumiwa zinaendelea
kwa kushirikiana na mume wake aliyefahamika kwa jina la LAUSI KIDAGILE,
Mkazi wa Sae kwani mara baada ya tukio hili mtuhumiwa ametoweka nyumbani
kwake.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya
Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA ninatoa wito kwa yeyote
mwenye taarifa zitakazofanikisha kukamatwa mtuhumiwa azitoe Jeshi la
Polisi ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yake. Aidha ninatoa wito
kwa wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa
za uhalifu na wahalifu ili kuzuia, kutanzua na kutokomeza vitendo vya
kihalifu.
Imesainiwa na:
[MOHAMMED R. MPINGA – DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
Post a Comment