Kitaifa, Kimataifa, Siasa, Michezo na Burudani

Mghwira amvaa Lowassa, asema kuhama chama ni ufisadi wa kisiasa

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema kuwa njia aliyoitumia aliyekuwa mgombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu uliopita kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa ilikuwa ni aina fulani ya ufisadi wa kisiasa.

Ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akifanya mahojiano na Gazeti la Mwananchi ambapo amesema kuwa Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema njia aliyoitumia ilikuwa ni aina mojawapo ya ufisadi kwakuwa hakupitishwa na chombo chochote ndani ya chama chake.

Amesema kuwa hata katika Kampeni za uchaguzi mkuu, Ukawa haikuzungumzia suala la ufisadi kwakuwa kiongozi huyo teyari alikuwa ameshajiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

“Kwenye Kampeni za mwaka 2015 chama kikuu cha upinzani (Chadema) hakikuwa tena kinazungumzia suala la ufisadi, labda kwa hofu kuwa mshtumiwa wa ufisadi alikuwa mgombea wao, kwa bahati mbaya wao ndio waliibua tuhuma za ufisadi, lakini kuondoka kwa Dkt. Slaa nako kulikuwa ni tatizo, ingawa watu hawakutaka kulifuatilia,” amesema Mghwira.

Aidha, Mghwira amesema kuwa watu walitakiwa kuhoji sababu za kuondoka kwa Dkt. Slaa na alikoelekea, nakuongeza kuwa ni ajabu kwa kiongozi anayepigania demokrasia anaingia kwenye chama na kugombea nafasi ya urais bila kupitishwa chombo chochote.

Hata hivyo, Mghwira ambaye ni kiongozi wa kwanza wa upinzani kushika wadhifa wa ukuu wa mkoa tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992, amesema kuwa njia waliyotumia Chadema si tu inarudisha nyuma siasa za upinzani, bali haikutoa picha nzuri ya demokrasia ndani ya upinzani.

Alikerwa kuvuliwa uenyekiti
Katika mahojiano hayo yaliyofanyika nyumbani kwake Shanty Town mjini Moshi, Mghwira alikumbuka karaha aliyoipata baada ya furaha ya kuaminiwa na Rais na kupewa wadhifa huo.

Alisema kama si ubabaishaji wa kisiasa Tanzania, asingeondolewa kwenye uenyekiti wa ACT-Wazalendo.

“Changamoto niliyokutana nayo ACT-Wazalendo kama mwenyekiti ni kukosa wigo sahihi wa kisiasa kwa sababu kama tungekuwa tunafanya siasa sahihi, nisingeondolewa uenyekiti,”alisema.

Mghwira alisema, “Naapishwa tu kuwa RC (mkuu wa mkoa) kesho yake naondolewa tena tukiwa tumepanga kukutana kwenye kikao na mpaka leo hatujawahi kukutana.

“Nimesoma kwenye magazeti kuwa mrithi wa Mghwira kutembelea mikoa saba, yaani na mrithi ameshapatikana. Hizo si siasa, huo ni ubabaishaji. Ubabaishaji wa kisiasa Tanzania ni tatizo,” alisema.

Aliongeza, “Sisi kina mama tukisimama imara tunaweza kuondoa dhana hii ya siasa za ubabaishaji. Ni siasa za kipuuzi kabisa. Mmekubaliana mkutane muongee, hamuongei wenzako wanakaa pembeni. Umechaguliwa na mkutano mkuu unaondolewa na kamati ndogo. Watu 370 karibu 400 hivi walikuchagua, siku ya kuondolewa unaondolewa na watu watatu au wawili au mmoja. Hiyo si siasa ni dalili tosha kuwa hakuna siasa.”

Alisema mbaya zaidi ni kuwa watu wanaokuondoa hawakutumwa na mkutano mkuu, wala hawakukaimishwa na kamati kuu.

Hakuna upinzani nchini
Baada ya kujumuisha yote hayo na hasa alivyotimuliwa kwenye uongozi, mkuu huyo wa mkoa akawa na jibu moja kuhusu siasa za upinzani, “Hakuna siasa za upinzani, bali zilizopo ni za kurudishana nyuma maendeleo.

“Siasa ni kitu kizuri kwa maana ya ile mijadala, kubadilishana mawazo na kuzungumzia masuala ya itikadi, mipango ya kijamii... hakuna hiki kitu Tanzania.”

Badala yake alisema, “Tumeweka siasa kama ni uhasama kati ya chama tawala kilichoshinda kihalali na vyama hivi vingine. Kila siku watu wanatafuta makosa ya wenzao (Serikali) hata kama inafanya vizuri. Hiyo sio siasa.

“Vyama vya upinzani hapa hatuendeshi siasa. Awali, chama chochote kitakachoibuka na siasa inayoeleweka kinaweza kutawala nchi hii kwa miaka 100 ilimradi tu kitoke na siasa inayoeleweka.”

Mghwira alisema, “Vikitokea vyama vitatu vinaendesha siasa inayoeleweka tunakuwa mahali pazuri zaidi. Kwa maana kwamba wale wakiongea jambo lao, hata kama hawatawali, mtawala asikie na kuthamini.

“Sisi hapa Tanzania kuna aina ya siasa za kudidimizana. Kwa sisi wanawake wanaharakati tunaziita PhD (pool her down). Unavutwa tu chini hutakiwi kukua. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii.”


Alisisitiza, “Kuna watu wanafikiri kwamba ili kitu kiwe sahihi ni lazima wao wakifanye (upinzani) lakini kikifanywa na watu wengine hakiko sahihi. Hiyo ni kutokuwa mwanasiasa. Kuwa mwanasiasa si kugombana ni kuwa na uwezo wa kujenga hoja, kuitetea na kuisimamia. Mwenzako akija na hoja kubwa zaidi kubali.”
Labels:

Post a Comment

[facebook]

MKRdezign

Contact Form

Name

Email *

Message *

Powered by Blogger.
Javascript DisablePlease Enable Javascript To See All Widget