Ujenzi wa Daraja la Kavuu lenye urefu
wa Mita 89 linalounganisha Halmashauri ya Wilaya ya Mlele na
Halmashauri ya Wilaya ya Mpwimbwe Mkoani Katavi ujenzi wake umekamilika
na litaanza kutumika ifikapo mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.
Akizungumza mara baada ya kukagua
ujenzi wa Daraja hilo Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
Eng. Edwin Ngonyani amesema kukamilika kwa ujenzi huo kutarahisisha
usafirishaji wa abiria na Mizigo kutoka Mkoa wa katavi kwenda mikoa ya
jirani.
“Serikali iliona kero kubwa
wanazozipata wananchi wa mkoa huu hasa kwenye usafirishaji wa abiria na
mizigo kwenye kipindi cha mavuno, hivyo baada ya kukamilisha Daraja hili
wananchi wataweza kupita vipindi vyote vya Mwaka,” alisema Naibu Waziri Eng. Ngonyani.
Aidha, Eng. Ngonyani amemuagiza Meneja
wa Wakala wa Barabara (TANROADS), Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi
Kuhakikisha Mzani unaohamishika unawekwa ili kudhibiti magari
yatakayozidisha Tani 36.
Kwa upande wake Meneja wa Wakala wa
Barabara Mkoa wa Katavi Eng. Abdon Maregesi amemuhakikisha Naibu Waziri,
Eng. Ngonyani kuwa wakala utaweka mzani huo ili kutoruhusu magari
yaliyozidisha Uzito wa Mzigo kupita kwenye Daraja hilo.
Wakati huo huo, Naibu Waziri Eng.
Ngonyani amekagua ujenzi wa Nyumba za Viongozi Mkoani humo na kuuagiza
Wakala wa Majengo nchini (TBA), kuhakikisha ujenzi wa nyumba hizo
unakamilika ifikapo Novemba mwaka huu.
“Serikali imeshatoa fedha za
kukamilisha ujenzi wa nyumba hizi, ujenzi huu ulisimama kwa takribani
miezi minne kwa sasa hakuna sababu ya ujenzi kusuasua wakati fedha zipo,
ninakuhakikishia Mkuu wa Wilaya nyumba hizi zitakamilika kwa wakati ili
zianze kutumika,” alisisitiza Naibu Waziri Eng. Ngonyani.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Eng.
Nyonyani amekagua ujenzi wa Barabara ya Sitalike-Mpanda yenye urefu wa
kilomita 36.9 ambao ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99, barabara
hii ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia Tunduma kupitia Sumbawanga,
Mpanda, Uvinza, Kibondo, Nyakanazazi hadi Mutukula.
Naibu Waziri Eng. Ngonyani yupo katika
Ziara ya kukagua Miundombinu ya barabara, Viwanja vya Ndege, Ujenzi wa
Nyumba za viongozi na Madaraja katika Mkoa wa Katavi.
Post a Comment