Serikali imesema itawalipa fidia kwa
mujibu wa sheria wananchi wote waliopisha ujenzi wa barabara katika
maeneo mbalimbali ya nchi.
Amesema hayo Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa wakati akizungumza na
wananchi wa Mwigumbi mkoani Shinyanga alipokagua ujenzi wa barabara ya
Mwigumbi – Maswa yenye urefu wa KM 50.3 inayojengwa kwa kiwango cha lami
na mkandarasi wa Kampuni ya CHICO na kuridhishwa na kasi ya ujenzi wake
ambao unagharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 61.
“Kila anayestahili kulipwa fidia
atalipwa kama sheria inavyoelekeza na endapo akatokea yeyote mwenye
malalamiko Serikali ipo itamsikiliza,” amesema Waziri Prof. Mbarawa.
Amewataka wananchi kutoa ushirikiano
kwa Mkandarasi na Viongozi wa Wakala wa Barabara (TANROADS), wa mkoa ili
kuhakikisha barabara hiyo inakamilika kwa wakati na spidi inayotakiwa.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amewahimiza
makandarasi wote nchini kutoa kipaumbele cha ajira kwa wakazi wa maeneo
husika inapopita miradi ya maendeleo ya ujenzi wa miundombinu
mbalimbali ili kuwapatia kipato na kuinua uchumi wao.
Naye, Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa
Shinyanga Eng. Batholomeo Ndirimbi, amesema mpaka sasa tayari fedha
zimetengwa kwa ajili ya ulipaji fidia na watahakikisha kuwa fedha hizo
zinalipwa kwa watu sahihi wanaostahili fidia hizo.
“Tutasimamia zoezi hili kwa umakini na kutoa fidia kwa wale wote wanaostahili kisheria,” amesema Eng. Ndirimbi.
Ameongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo umefikiwa asilimia 77 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof.
Mbarawa amekagua mradi wa ujenzi wa barabara ya Usagara-Kisesa KM 16.1
inayojengwa kwa kiwango cha lami ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 75
na daraja la Nyashishi lenye urefu wa mita 67.9 ambalo ujenzi wake
umekamilika kwa asilimia 99.5 mkoani Mwanza.
Kwa upande wake, Meneja wa TANROADS
Mkoa wa Mwanza Eng. Marwa Rubirya, amesema ujenzi wa barabara hiyo
unaendelea vizuri na mkandarasi atamaliza kwa wakati uliopangwa na
viwango walivyokubaliana katika mkataba.
Ameongeza kuwa barabara hiyo inapita
katika wilaya mbili ambazo ni Misungwi na Magu na kukamilika kwa
barabara hiyo kutarahisisha huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo
katika wilaya hizo na mikoa jirani.
Post a Comment